Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ibada Ijumaa Kuu, Pasaka kufanyika Dar

9f28da9d296fb2d58e68eee76d90b87b.jpeg Ibada Ijumaa Kuu, Pasaka kufanyika Dar

Fri, 2 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

IBADA ya Ijumaa Kuu kitaifa inafanyika leo katika Kanisa la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) linalotumiwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Ibada hiyo ni kumbukumbu ya kifo cha Yesu Kristo.

Aidha Misa Takatifu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka, inayoadhimishwa kukumbuka Ufufuko wa Yesu Kristo, itafanyika kitaifa katika Parokia ya Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Ibada zote hizo mwaka huu nchini, zinafanyika katika kipindi cha maombolezo ya kitaifa kutokana na kifo cha Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungabno wa Tanzania, John Magufuli, hivyo dua, sala na maombi vitaelekezwa kumuombea.

Ofisa Habari wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji John Kamoyo, alisema jana kuwa, ibada hizo pia zitatumika kumwombea hekima Rais wa Sita wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Baraza la Mawaziri Tanzania.

Akizungumza na HabariLEO jana, Mchungaji Kamoyo alisema ibada ya leo inaongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa chini ya taratibu za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na inaanza saa 9 alasiri hadi saa 12 jioni.

“Jumapili misa kitaifa itafanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya

Msimbazi. Itaanza saa 2:30 asubuhi na itaongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Yuda Thaddeus Ruwai’chi,” alisema Mchungaji Kamoyo. Alisema ibada hizo pia zitaendelea kutumika kuiombea nchi amani, utulivu na mshikamano.

“Wakati huu wa majonzi tuendelee kumuomba Mungu atufariji na kututia nguvu, upendo zaidi, kumuombea Rais mpya Mungu ampe hekima na maarifa, kama tulivyoona jana (juzi) ameboresha Baraza la Mawaziri, Mungu awape utendaji ulio bora,” alisema Mchungaji Kamoyo.

Aliwaomba Wakristo nchini wajitoe kuendelea kuwaombea viongozi kwa Mungu ili wayaenzi mazuri ya Rais Magufuli ili umoja na amani ya nchi viendelee.

Chanzo: www.habarileo.co.tz