Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakuna mwanadamu aliyezaliwa awe maskini- Mchungaji Komba

Hakuna mwanadamu aliyezaliwa awe maskini- Mchungaji Komba

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakuna mwanadamu amezaliwa ili awe masikini, isipokuwa mtazamo na juhudi zake ndizo huamua kikomo cha mafanikio yake.

Hayo yamesemwa na Mchungaji, Amosi Komba wa Kanisa la Ufufuo na Uzima leo Jumatano Desemba 25, 2019 wakati wa misa ya sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo ijulikanayo kama Sikukuu ya Krismasi.

“Geuka sasa, geuza fikra zako sasa, geuza mtazamo wako sasa. Wewe ni mtu muhimu sana ukijitambua,” alinukuu wakati akihubiri injili kanisani hapo.

Wafuasi waliitikia kwa kuinuka kwenye viti vyao wakipiga makofi na akina mama vigelegele, wakati Mchungaji Komba alipoendelea kusema kuwa Mungu hujibu kwa wakati usio tegemewa na huwainua walio na fikra chanya katika kipindi chochote.

“Wapo watu wanaishi katika mazingira ambayo wanajiona wametengwa, wananyanyaswa, wanasemwa vibaya na kuhisi wao ni wa hivyohivyo. Ngoja nikwambie leo kuwa wewe ni ‘special’ (muhimu) sana endapo utageuza fikra zako na kujitambua,” alihubiri.

Akitoa mfano wa kuinuliwa kwa nabii Mussa, mchungaji alisema kuwa kama ambavyo Musa aliinuliwa na Mungu akiwa mchungaji tu wa kondoo jangwani ndivyo anavyowainua binadamu wengine wakati wakiwa katika hali za chini.

“Musa alikuwa ni mtu wa kujificha kutokana kesi ya mauaji yaliyokuwa yanamkabili. Aliishi ukweni kwake akichunga kondoo wa baba mkwe wake lakini Mungu alimuinua na akawa mtawala wa watu wote wa Israeli,” alinukuu.

Pia aliongeza kuwa, hata Yesu mwenyewe alizaliwa katika zizi la ng’ombe tu kama mtu wa chini sana lakini akaja kuwa mtu muhimu sana duniani.

“Nataka ubadili fikra zako kuanzia leo. Nataka ujue unaweza kufanya biashara, kujenga nyumba na kumiliki magari na mali nyingi tu,” aliwaambia waumini.

Akitoa ujumbe wake mkuu wa sikukuu ya Krismasi Mchungaji Komba alisema kuwa ‘Mahali pasipotegemewa ndipo pamejawa neema.

Dickson Julius, mkazi wa kinondoni ni muumini wa kanisa hilo ambaye amesema injili ya leo imempa mwamko wa kutokata tamaa.

“Nilikuwa na makwazo na magumu sana mwaka huu, hususani madeni na ugumu wa maisha lakini najiona kama mpya na nitapigania sana maendeleo na afya yangu mwaka 2020,” alilimbia Mwananchi baada ya ibada.

Alisema anajiona wa thamani na anaamini akibadili fikra zake mgando alizokuwa nazo awali anaweza kufanya mambo makubwa sana.

Pia, Theodora Peter mkazi wa Ubungo na muumini wa kanisa hilo aliliambia Mwananchi kwamba yeye alijiona ni wa kawaida sana lakini amegundua kuwa ni wa kipekee sana baada ya mahubiri.

“Nimekuwa nikiona mambo yangu mengi hayaendi nikahisi nina mikosi lakini leo nagundua kuwa huenda ni mtazamo tu au bado Mungu hajaamua niyatakayo yatimie kwa muda huu,” alisema akiongeza kuwa hajakata tamaa na anaamini atafanikiwa mwakani.

Chanzo: mwananchi.co.tz