Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya sheikh aliyetoweka yaililia polisi

31884 Sheikh+pic TanzaniaWeb

Mon, 17 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Siku 11 tangu alipotoweka Sheikh Bashir Gora, ambaye ni mkuu wa Chuo cha Kiislamu Nyakato jijini hapa, familia yake imendelea kuweka matumaini kwa vyombo vya dola, huku polisi wakiwatahadharisha watekaji.

Sheikh Gora alitekwa Desemba 6 na watu wasiojulikana baada ya kijana mmoja kwenda chuoni hapo kuulizia nafasi za kujiunga kwa ajili ya mdogo wake akidai ameagizwa na baba yake.

Akizungumza na Mwananchi, mke mdogo wa Sheikh Gora, Farida Rashid alisema wamewekeza matumaini yao kwa polisi kwa sababu wao hawajui pa kuanzia.

Alisema kadri siku zinavyokwenda ndivyo wanapata wakati mgumu kutokana na kuwa ndiye tegemeo lao kwa kila kitu kwenye familia zake mbili zenye wake wawili na watoto saba.

“Tunaona siku zinapita hatujui kama yupo salama au la maana waliomchukua hatukujua walikuwa na nia gani mpaka wampoteze siku zote hizi. Sisi tupo tu nyumbani hatuna hata biashara tunayofanya, halafu watu wanamchukua mtu kama huyo,” alisema Farida.

Mmoja wa watoto wa Sheikh Gora, Sabra Bashir alisema, “Tunaomba wamrudishe baba, tunamhitaji kwani hata tukianza masomo hakuna wa kutulipia ada.”

Mmoja wa marafiki wa familia hiyo, Khalifa Issa alisema licha ya Sheikh Gora kutegemewa na familia, pia anategemewa na jamii kwa sababu ni kiongozi wa dini.

Alisema kutoweka kwake kunaweza kusababisha familia ikapata matatizo makubwa kwa kukosa matunzo muhimu huku watoto wakitakiwa kwenda shule mwezi ujao.

“Huyu alikuwa mtu wa watu, sikuwahi kusikia kama ana ugonvi na mtu, kwa kweli kitendo hiki kinatusikitisha sote. Siku zote baba ndiye muhimili wa familia, hivyo (asipopatikana) huenda hata familia ikatetereka kwa sababu ya utashi wa watu fulani, jambo hili linamuumiza kila mmoja,” alisema Issa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jonathan Shanna: “Bado tunawasaka (waliomteka) na niwatumie salamu watu hao wamuachie, vinginevyo popote walipo tutawakamata.”



Chanzo: mwananchi.co.tz