Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Nyamagana asitisha ibada za kanisa la mhubiri Zumaridi

84979 Kanisa+pic DC Nyamagana asitisha ibada za kanisa la mhubiri Zumaridi

Thu, 21 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Serikali ya Tanzania imesitisha ibada katika kanisa la mchungaji Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi  lililopo mtaa wa Iseni kata ya Butimba jijini Mwanza.

Uamuzi huo umetolewa jana Jumatatu Novemba 18, 2019  baada ya malalamiko ya watu mbalimbali kuhusu ibada za mhubiri huyo ambaye pia hujiita Mungu wa duniani.

Amri hiyo inayohusisha pia ibada za majumbani imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Philis Nyimbi mbele mchungaji  huyo na waumini wake.

Baada ya amri hiyo kutolewa mchungaji huyo hakuwa tayari kueleza chochote.

"Mimi sina cha kusema. Siwezi kuzungumza chochote kwa sasa," amesema mchungaji Diana alipotakiwa kutoa maoni yake

Nyimbi amesema uchunguzi wa kina wa Serikali umebaini kuwa licha ya ibada, maneno na mafundisho yanayotolewa kanisani hapo kukiuka sheria na misingi ya imani, kanisa hilo  linatumia usajili wa kanisa jingine la Pentecostal Christian of  Tanzania.

“Kiongozi wa Kanisa hili anajiita baba na mfalme wakati yeye ni wa jinsi ya kike,” amesema Dk Nyimbi.

Amesema baadhi ya vitendo ambavyo hata hivyo hakuvitaja vinavyofanywa na kiongozi wa kanisa hilo vina athari na madhara kwa waumini na watu wengine.

“Serikali imebaini kiongozi wa kanisa hili anaendesha ibada kinyume na sheria ya usajili wa vyama au jumuiya za kijamii sura 337 kwa kupotosha umma kwa kujiita Mungu wakati yeye ni binadamu au baba na mfalme wakati yeye ni mwanamke.”

“Kwa mamlaka niliyopewa kwenye sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 kifungu cha 14, 15, 16, vinavyosema punde tunapobaini kikundi au taasisi ina viashiria vya uvunjifu wa amani, mara moja tunapaswa kuchukua hatua,  nasitisha shughuli zote za ibada kanisani na nyumbani kwa mchungaji Diana,” amesema  Dk Nyimbi.

Amesema kabla ya kufikia uamuzi huo, ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wa taasisi nyingine za kidini kuhusu matendo ya kukiuka maadili na mafundisho ya  dini ya kiongozi wa kanisa hilo.

Pamoja na kusitisha shughuli zote za ibada kanisani na nyumbani, mkuu huyo wa Wilaya pia amesema Msajili wa Vyama vya Kijamii anaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu utendaji na uendeshaji wa kanisa hilo kabla ya kuchukua hatua zaidi za kisheria.

Mjumbe mstaafu wa Serikali ya Mtaa wa Iseni, Asha Adam amepongeza uamuzi huo wa Serikali na kutaja baadhi ya matukio ya kustaajabisha yaliyokuwa yakitendeka kanisani hapo kuwa ni pamoja na waumini kulala chini huku kiongozi wao huyo akiwakanyaga na kupita juu yao.

“Kuna wakati wanatoka kanisani na kwenda kulala na kujigaragaza kwenye matope wakidai kumshambulia shetani, kuna mambo ya ajabu yalikuwa yanatendeka hapa na hakika Serikali imechelewa kuchukua hatua,” amesema Asha

 

Chanzo: mwananchi.co.tz