Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DARASA LA RAMADHANI Mambo ya kuzingatia  mwezi wa Ramadhani 

C64a78e2886b27af56c922d03376bae7 DARASA LA RAMADHANI Mambo ya kuzingatia  mwezi wa Ramadhani 

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JANA Waislamu wa Tanzania walianza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani baada ya kumalizika kwa mwezi wa Shaaban huku wale wanaofuata mwandamo wa mwezi kimataifa wakiwa wameanza kufunga tangu juzi.

Je, kwa nini Waislamu wanafunga? Kufunga ni kutekeleza Amri ya Mwenyezi Mungu ambaye anasema katika Kuran: "Enyi mlioamini, mmeamrishwa (mmelazimshwa) kufunga (swaumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu (Kuran 2:183).

Kwa hiyo utaona ibada hii kwa mujibu wa Kuran, hawakulazimishwa waislamu wa leo pekee bali hata jamii zilizotangulia.

Je, kwa kufunga mtu anapata nini? Mwenyezi Mungu anajibu kwenye aya hiyo anaposema: Fungeni ili mpate kuwa wachamangu.

Tafsiri pana ya hapa ni kwamba kufunga ni kambi ama darasa ambamo Waislamu wanapaswa kuingia kwa ajili ya kumcha Mungu kwa wingi na kwa juhudi nahivyo watakapotoka humo wawe wameiva kiuchamungu na siyo kushinda na njaa kwa maaana ya kufunga kwa mazoea au kufuata mkumbo.

Yaani, kila mwaka Waislamu wanapata wasaa wa mwezi mzima wa ‘kujifua’ katika suala zima la uchamungu wao na inatazamiwa kwamba wanapotoka kwenye chuo hiki cha funga waendelee na uchamungu hadi kwenye chuo kingine, yaani Ramadhani nyingine kwa wale watakaojaaliwa kufika.

UCHAMUNGU NI NINI?

Uchamungu ni sentensi fupi yenye maelezo marefu. Lakini kwa kifupi uchamungu ni kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na mkatazo yake. Yaani kila anachokifanya mfungaji kinapaswa kiwe kinachunga mipaka aliyoelekeza Mwenyezi Mungu.

Mwanazuoni mmoja anaeleza mambo manne yanayohusu uchamungu ambayo ni; kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu, kufanya kila linalomridhisha Mwenyezi Mungu, kuchuma au kula vya halali na mwisho ni kuishi kwa kujiandaa kila wakati kwamba utaondoka duniani muda wowote na hivyo ukutane na mola wako ukiwa salama.

Tafisri nyingine ya uchamungu ni kuhakikisha kila saa, dakika hadi sekunde unafanya yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu. Ukiona jambo unalofanya haliridhiwi na muumba wako basi ujue umekengeuka uchamungu.

Kwa hiyo mfungaji anapaswa kujipima kwa kujiuliza haya maswali: Je, yale ambayo Mwenyezi Mungu alioamrisha kufanya anayafanya? Yale aliyotaka yaachwe mfungaji anayaacha? Kama mfungaji atafunga ama kumaliza mfungo na bado hajaacha maasi sambamba na kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu basi kwa mafundisho hayo ajue anafunga kwa mazoea na lile lengo la kufunga linakuwa halijatimia kwake.

Ni vyema kila anayefunga akajiangalia nafsi yake na kama alikuwa anafunga kwa mazoea abadilike sasa.

Mafundisho yanaonesha kwamba maswahaba wa Mtume (SAW) na wema waliotangulia walifahamu sababu ya kuumbwa kwao. Walijitambua kwa nini wako duniani na nini kitakuwa mwisho wa maisha yao hapa duniani na kisha wakatekeleza yale waliotakiwa kufanya na kuacha yale waliokatazwa. Hawa walikuwa wanafikia lengo la uchamungu.

FAIDA ZA UCHAMUNGU

Faida za uchamungu pia zipo nyingi na hapa zinatajwa chache. Kubwa ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kumuingiza mja kwenye pepo yake. Mwenyezi Mungu anasema kwamba fanyeni haraka kukimbilia msamaha wake na mfanye haraka kuipata pepo yake. (Kuran 3:133).

Ili kupata pepo ya Mwenyezi Mungu na msamaha wake lazima Muislamu ‘ajipinde’ sana hususani katika mwezi huu mtukufu.

Kadhalika Mwenyezi Mungu anasema kwamba pepo imeandaliwa wachamungu (na moto kwa wanaomuasi). Hivyo, Muislamu anapofanya ibada, kuswali, kufunga, kutoa zaka, kwenda kuhiji na ibada zingine huwa matarajio ya kupata pepo ambayo ni maisha ya milele na siyo kufanya hayo kwa ajili ya kujionesha kwa wanadamu.

Kwa hiyo ni vyema mfungaji na kila anayemuamini Mwenyezi Mungu ajue kwamba kupata pepo si jambo rahisi. Ni lazima ajitahidi kumcha Mwenyezi Mungu kwa kutimiza maamrisho yake.

Kwa mantiki hiyo, mtu asione kuamrishwa kufunga mwezi wa Ramadhani ni kama hatua ya Mwenyezi Mungu kampa uzito. Anayedhani hivyo, huyo hajajitambua. Ni kwamba mfungaji anaumia leo lakini kesho atapata pepo na bila shaka hakuna Muislamu ambaye hataki pepo.

Mwenyezi Mungu anasema hakika vipenzi vyake hawatakuwa na hofu katika maisha ya dunia wala ahera. Hawa hawatumuogopa yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu tu na wala hawatuhuzunika siku ya kiama. (Kuran 10:63)

Leo hii ukikutana na watu wengi utaona wanahofu za kidunia na si Mungu wao. Mtu anakuwa na hofu ya kufukuzwa kazi, hofu ya kuzaa watoto wengi, hofu ya kuoa wake wengi (wanaume), lakini yote hii ni kukosa uchamungu kwa maana ya kumtegemea kwa dhati kabisa Mwenyezi Mungu mtukufu.

Mchamungu hata akipata matatizo ama maradhi anajua ni sehemu ya mitihani tu ya Mwenyezi Mungu na ndipo anakuwa karibu zaidi na muumba wake kwa sababu anajua ni sehemu ya mtihani.

Mchamungu pia huwa na huruma na mwema kwa wanzake na hivyo pia hupata manufaa ya kidunia kutokana na wema wake.

YA KUFANYA KWA MFUNGAJI

Ifahamike kwamba kufunga, mbali na kuacha kula na kunywa kuanzia dakika chache kabla ya kuingia alfajiri ya kweli hadi kuchwa kwa jua (magharibi), Muislamu anatakiwa pia kufunga macho yake yasiangalie machafu, kufunga mdomo wake kutosema uongo, kusengenya na kufitinisha na masikio yake kuyafunga dhidi ya kusikia machafu na upuuzi.

Katika mwezi huu ambao ndio kwanza umeanza, kila aliyefunga anatakiwa kuzidisha ibada kwa maneno na vitendo. Walioghafilika huko nyuma wazinduke na kuifanya Ramadhani hii kama kitu cha kuwababadilisha.

Kadhalika kila mwenye chochote ajitahidi katika kutoa sadaka, kusaidia wenye shida, kusalimia wagonjwa na kila jambo lenye heri. Ni vizuri ifikie matendo ya kila aliyefunga mwezi huu yawavute hata wasio Waislamu. Kwa kifupi mfungaji anatakiwa kuwa mwema na mwenye huruma kwa binadamu wenzake bila kujali dini zao.

Walete toba kwa wingi, wasimame sana usiku kwa kufanya ibada na kumtaja sana Mwenyezi Mungu kwa sababu huu ndio mwezi wa kuchuma thawabu kwa wingi. Wakati miezi ya kawaida mtu akifanya jambo jema moja analipwa hadi thawabu 10, mwezi huu thawabu zinafika hadi zadi ya 700 kwa jambo moja la heri.

Shehe Abdulqadir al-Ahdal, Rais wa Al-Hikma Foundation anasema katika moja ya hotuba zake za Ijumaa kwamba wakati mja anaweza kunyang’anywa thawabu zake siku ya Kiyama kwa kulipwa wale aliowadhulumu, thawabu za Ramadhani hazihusishwi na hilo.

MAMBO YA KUEPUKA

Kama ilivyokwisha dokezwa, kufunga hakuna maana ya kuacha kula na kunywa pekee, bali pia mfungaji anatakiwa kuacha maasi yote. Aache kusema uongo, kusengenya, kuiba, kudhulumu, kuzini na maovu mengine.

Matendo hayo hayafai siku zote lakini katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani anayeyafanya huandikiwa madhambi maradufu.

KUFUNGA BILA SWALA

Waislamu wengi wanaipa heshima ibada ya funga na kuitekeleza ibada ya swala. Hili ni kosa kubwa kwa mfungaji, na ingawa hizi ni ibada mbili tofauti lakini huenda funga ya asiyeswali ikawa ya mashaka kukubaliwa.

KURUDIA MAASI

Anayefanya ibada ya Ramadhani pekee na ikiisha anarudi kwenye maasi huyo hajajua lengo la kuumbwa kwake na kufanya ibada. Kimsingi, kama ilivyoelezwa hapo juu, Ramadhani ni kambi au chuo ambacho humfanya mtu abaki mcha-Mungu. Ramadhani ni sawa na msimu wa kulima kwa matarajio ya kuvuna baadaye.

Kuna watu wanadhani wamekuja hapa duniani, kula, kunywa na kustarehe. Hawajiulizi wale waliotangulia mbele ya haki; babu zao, bibi zao na hata wazazi wao wako wapi na kule walikotangulia kuna nini kinachoendelea.

Mwezi huu unatakiwa umsaidie kila aliyefunga kuhuisha moyo wake kwa kutenda mema. Anayerudi kwenye maasi baada ya Ramadhani, ni sawa na mkulima anayechoma shamba lake baada ya kustawi vyema na hivyo wakati wa mavuno (kiyama) atakuwa na majuto mkubwa.

Sababu kubwa ya watu kurejea kwenye maasi baada ya Ramadhani ni kukosa hofu ya Mwenyezi Mungu. Mtu wa aina hiyo hajui nafasi ya Ramadhani na ndio hao wanaofunga kwa mazoea.

Kuthibitisha hilo, utaona siku hizi za mwanzo za Ramadhani, watu watajaa misikitini lakini kadri siku zinavyokwenda watakuwa wanapungua. Hii ni tofauti na waliotangulia ambao kadri mwezi ulivyokuwa unayoyoma ndivyo wanavyojifunga kibwebwe na kusikitika kwa nini unaisha mapema na hivyo kukaa msikitini kila wanapokuwa na wasaa.

DHIMA YA MAIMAMU

Katika mwezi huu ni vyema maimamu na wahadhiri wakajitahidi kuwafanya Waislamu wabaki misikitini.

Moja ya mbinu ni kuwafanya waujue ukubwa wa Mwenyezi Mungu sambamba kuwawezesha kuwa na hofu ya Mungu.

Maimamu wawasaidie waumini wao kujua kwa uhakika hapa duniani ni sehemu ya kupimwa matendo yetu. Hilo lifanyike si kwa maneno makali kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka watu walinganiwe dini kwa hekima na mawaidha mazuri kwa sababu baadhi ya watu nyoyo zao ni dhaifu.

Itaendelea

Chanzo: www.habarileo.co.tz