Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Buhembo alivyokiona kifo chake

Buhembo alivyokiona kifo chake

Mon, 16 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwalimu na mtunzi wa muziki wa injili nchini Clement Buhembo maarufu kama Papaa aliyefariki dunia juzi asubuhi ni kama vile alikitabiri kifo chake.

Buhembo alifariki katika Hospitali ya Kanisa la African Inland Church (AIC), Makongoro jijini Mwanza alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuishiwa nguvu ghafla na kukimbizwa hospitali.

Buhembo ni mwalimu maarufu wa kwaya, aliyetunga nyimbo kama ‘Chezea pengine, usichezee amani’ iliyo kwenye albamu ya Keusi ya kwaya ya Vijana AIC Makongoro, Mwanza.

Alipata umaarufu kupitia albamu ya Kekundu lakini pia alikuwa akifundisha kwaya mbalimbali nchini ikiwamo kwaya ya Vijana Chang’ombe (CVC) Dar es Salaam.

Diana Buhembo binti wa kwanza wa marehemu, alisema baba yake alikuwa kama anahisi atafariki.

“Hospitali aliyolazwa ipo humu ndani ya kanisa, hivyo watu wengi walikuwa wanakwenda kumuona, neno alilokuwa akilirudia mara kwa mara ni kuwataka wapendane na kila mmoja amhurumie mwingine ili wanakwaya wawe na ushirikiano.

“Pia alihimiza ushirikiano kwa waumini ili kuimarisha mshikamano kanisani,” alisema Diana na kuongeza kuwa kwa watu waliokwenda kumuona usiku alikuwa akiwaomba watoke ili azungumze na Mungu.

Alisema kijana aliyelala naye usiku wa kuamkia Jumatano aliwaeleza kuwa mara kadhaa alimuomba atoke nje ili azungumze na Mungu.

“Nilikuwa msibani Bariadi, tena alinisisitiza sana niende kwenye mazishi, lakini nilizungumza naye Jumatano usiku nikamuuliza niende hospitali akasema niende nyumbani nikapumzike ila niwahi kumpelekea nguo za kubadilisha asubuhi, hilo halikutimia akawa amefariki.

“Mwanakwaya mwenzetu Ezekiel Maela ndiye aliyelala naye usiku huo na alitueleza kuwa baba alimwambia ampishe azungumze na Mungu zaidi ya mara mbili usiku na aliporudi alimkuta anazungumza mambo ya kiimani utadhani kuna mtu ilihali wapo wawili,” alisema Diana.

Alisema taarifa za awali kutoka kwa wakubwa wa familia yao, mazishi yatafanyika Jumatatu na kwa sasa msiba upo kanisani Makongoro ambako ndipo walipokuwa wakiishi.

Diana alisema baba yake hakuwa akiumwa wala hana historia ya kubanwa na kifua, aliamka mzima asubuhi na akampa dawa ya meno ili apige mswaki kwa ajili ya maandalizi ya kwenda kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza.

Alisema, “Baba alituambia tutangulie yeye atakuja na mwenyekiti wa kwaya wa vijana AIC ya Makongoro na mzee mwingine anaitwa Songola.

“Tukatangulia, tukiwa uwanjani saa tatu asubuhi tukaambiwa baba ameishiwa nguvu na amepelekwa hospitali, tulipomaliza shughuli na kuja kumuona tukaambiwa vipimo vinaonyesha ana malaria tatu na yeye mwenyewe akasema kifua kinambana, ”alisema Diana.

Alisema hakuwa na hali mbaya na aliwaambia anamalizia sindano siku inayofuata angeruhusiwa, “Ndiyo maana amezungumza hadi dakika chache kabla ya kufariki, hakuwa anaumwa sana.

Chanzo: mwananchi.co.tz