Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi TALGWU kortini mashitaka ya mil 400/-

3a6b1aa6f3475abddb66893e0d925981 Bosi TALGWU kortini mashitaka ya mil 400/-

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

ALIYEKUWA Mkuu wa Kitengo Cha Uhasibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), Sospeter Omollo, amefi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashitaka 48 ikiwemo kughushi, ubadhirifu na utakatishaji fedha zaidi ya Sh milioni 400.

Omollo alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Luboroga, huku upande wa mashitaka ukiwakilishwa na Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hassan Dunia, akisaidiana na Lupyana Mwakatobe.

Mwendesha Mashitaka Dunia alidai katika shitaka la kwanza hadi la 46, mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa ya kughushi. Ilidaiwa kuwa kati ya Septemba 22, 2015 na Juni 5, 2017 katika benki ya BOA Tawi la Ilala kwa nia ovu, alighushi hundi 46 zenye thani ya Sh 410,170,000 Alidai kuwa katika shitaka la 47, mshitakiwa anakabiliwa na kosa la ufujaji na ubadhirifu.

Ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Septemba 22, 2015 na Juni 5, 2017 katika benki ya BOA Tawi la Ilala akiwa ni mhasibu alipokuwa ameaminiwa kama mtumishi, alifanya ubadhirifu wa Sh 410,170,000.

Katika shitaka la mwisho, mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kutakatisha Sh 410,170,000, kosa analodaiwa kulitenda katika tarehe tofauti kati ya Septemba 22, 2015 na Juni 5, 2017 katika Benki ya BOA Tawi la Ilala.

Alitakatisha fedha hizo huku akijua ni mazao ya makosa tangulizi ya ufujaji na ubadhirifu. Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kesi hiyo itarejea mahakamani Februari 16 mwaka huu kwa ajili kusomewa maelezo ya awali.

Mshitakiwa alipelekwa mahabusu kwa sababu shitaka la utakatishaji halina dhamana. Wakati huohuo, mkazi wa Tabata, Lina Muro (46) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 43.95.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi , Agustina Mbando baada kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi saba na kujiridhisha pasipo kuacha shaka yoyote.

Ilidaiwa kuwa Januari 26, 2018 katika maeneo ya Tabata Bima NSSF, mshitakiwa huyo alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 43.95. Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mbando alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wote saba pamoja na vielelezo, Mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka hivyo inamtia hatiani.

Hakimu Mbando alisema kutokana na ushahidi wa upande wa mashitaka uliotolewa, Mahakama inamtia hatiani hivyo atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na kutaifisha simu nne alizokutwa nazo.

Wakati huo huo, Hakimu Mbando aliwahukumu watu wawili wakazi wa Mbezi kwenda jela miaka 20 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuharibu miundombinu ya simu na kusababisha hasara ya Sh milioni 25 kwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL).

Washtakiwa hao, Rogers Festo (29) na Shafii Nampembe (43) walidaiwa kuwa Septemba 16, 2018 katika maeneo ya Mbezi, waliharibu miundombinu ya simu ya TTCL kwa kukata nyaya na kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Chanzo: habarileo.co.tz