Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bila hekima na akili, utajiri hauna faida

28722 Pic+mahubiri TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Naitwa Mchungaji Christosiler Kalata kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Usharika wa Mbezi Beach, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Ni Jumapili nyingine njema ninayokuletea neno la Mungu kupitia makala hii.

Neno la leo linatoka katika kitabu cha Mithali 3:13-16 likisema: “Heri mtu yule aonaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.”

Ni muhimu sana kufahamu kuwa kabla ya kuanza kufikiri kuhusu vyanzo vya kifedha na upatikanaji wa mitaji ya miradi mbalimbali iwe mikubwa au midogo, lazima ujihoji maswali kadhaa! Je, mimi nina hekima na akili?

Jiulize kama utapewa pesa, kwa mfano dola 1,000 (za Marekani) na hekima utachagua nini? Kwa haraka haraka wengi wetu watachagua dola 1,000, au fedha ya kiwango chochote kile, bila hekima pesa yoyote itakayoangukia mikononi mwako itakuwa haina thamani y0yote ile kwako.

Ni muhimu kufahamu kuwa utajiri na mtaji mkubwa zaidi kuliko vyote ni hekima na akili.

Mtu aliye na hekima na akili, ukisoma ule mstari wa kumi na sita. “Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.”

Wakati wote Mungu akiwaweka watu wa jinsi hiyo juu na kuwaimarisha. Yusufu aliwekwa juu kusimamia miradi mikubwa sana kule Misri, hadi leo anakumbukwa katika maandiko matakatifu, sababu ni kuwa Mungu alikuwa amempa hekima.

Farao akawaambia watumwa wake: “Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. “Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe,” Mwanzo 41:38-40.

Hekima na akili ni vitu vinavyomweka Mungu mbele, mtu akiwa na uchumi mzuri kisha asimweke Mungu mbele, huweza kupokonywa mali na mitaji aliyonayo haraka. Wakati mmoja, katika mkutano, mtu mmoja akamwambia Bwana Yesu: “Mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.

Akamwambia, mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa muamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyonavyo,” Luka 12:13-15. Tunaweza kuwa na hekima kwa kuomba. “Lakini mtu wa kwenu, akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu…” Yakobo 1:5.

Mungu anafahamu kuwekeza mtaji mkubwa kwa mtu mpumbavu, kuna uwezekano mkubwa wa kusambaratika, na mtu huyo kuingia katika uharibifu mkubwa. Kuna watu Mungu aliwapa kamtaji kadogo mambo yalipoanza kuchanganya, anaanza kunyanyasa watu. “Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri,” Mithali 21:17.

Mtu ambaye hana hekima, atafanya mambo ya ajabu ili kuonyesha watu kwamba amebarikiwa! Wazo la kuzalisha tena kwa mali aliyonayo anakuwa hana, wazo alilonalo ni kujipongeza. Bila hekima ya Mungu utajiri au fedha ni msiba mtupu. Shetani huweka mkono wake dhidi ya miradi ya watu wa Mungu. Nihitimishe kwa kusema neno hili, shetani humtumia mwanadamu kuleta uharibifu kama alivyo adui kwa Mungu ni adui mkubwa katika uchumi wa mtu binafsi, familia, kaya, na nchi.

Watu wakombolewe fikra zao, hapa nina maana ukombozi wa fikra, ili kuweza kutoka hatua moja na kwenda hatua nyingine ya maendeleo. Kila mwananchi wa Tanzania leo hii ukimuuliza unataka nini atakwambia “maendeleo”, Mtanzania ameanza kuyaona maendeleo, wakati akiendelea kujiuliza nini kimetokea katika miaka 50 toka kupata uhuru, nini kinakwamisha kupiga hatua za maendeleo, fahamu zake zinaanza kufunguka na kujua kumbe shetani anao uwezo wa kushambulia uchumi wa nchi.

Shetani alishambulia miradi ya Ayubu nia yake ilikuwa Ayubu aweze kumkufuru Mungu. Fahamu kwamba shetani anatumia akili ya mwanadamu kumvuruga asifikie malengo ambayo Mungu amemwekea kuyafikia.

Tanzania ni moja ya nchi ambayo mara baada ya kupata uhuru ilianzisha viwanda vingi, iliweza kuzalisha bidhaa bora Afrika Mashariki. Vimeenda wapi. Leo hii unaweza kusikia kiwanda cha kubangua korosho kimefungwa, korosho zinaenda kubanguliwa nje.

Hili jambo ni la kushangaza, utasikia kiwanda cha chai kimefungwa wakulima wanahangaika, pamba, alizeti, kahawa, kokoa, mkonge, matunda, mazao ya nafaka, mahindi, ngano, karanga, zabibu, mazao ya baharini, nani amewazuia Watanzania kuwa na viwanda vya kusindika mazao haya?

Shetani anaweza kukushambulia kwa maneno ya uongo kazini kwako kusudi upoteze ari ya kazi mwisho uipoteze na kazi yenyewe! Adui mwingine wa uchumi ni madeni. “Tajiri humtawala maskini, naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye,” Mithali 22:7.

Watanzania wengi, wanastaajabu, wanapoona uwezo wa kukusanya kodi kutoka watu ambao kwa miaka mingi utamaduni wa kulipa kodi kwao ulikuwa umetoweka kabisa! Ni wakati mzuri kwa Mkristo, Mtanzania kuamua hekima na akili itawale maisha yao, na kumpa Mungu utukufu.

Maadili mema, sala na dua, kumheshimu Mungu, kupendana, kutadumisha amani, na kuacha vitendo vya rushwa na ufisadi, kutaipeleka nchi hii katika maendeleo.

Chanzo: mwananchi.co.tz