Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barabara ya Jangwani-Magomeni yafunguliwa baada ya kufungwa

56688 Pic+barabara

Fri, 10 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam  imefunguliwa baada ya kufungwa saa 5:40 asubuhi.

Barabara hiyo ilifungwa saa 5:40 asubuhi na kufunguliwa saa 8:00 mchana leo Ijumaa Mei 10, 2019 kutokana na maji kujaa kwenye daraja la Jangwani na kupita juu ya barabara.

Akizungumza kwa simu Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Marson Mwakyoma, amesema walifunga barabara hiyo kwa muda kutokana na maji kujaa barabarani.

Mwakyoma amesema kwa kawaida mvua zikinyesha daraja hilo hujaa maji na kufurika hadi barabarani jambo linalosababisha eneo lote kujaa maji.

"Polisi imelazimika kufunga barabara kipande cha Magomeni na Jangwani baada ya eneo la Jangwani kujaa maji na kupita juu ya daraja, jambo ambalo lingeweza kusababisha maafa,” amesema Kamanda Mwakyoma.

Pia, Mwakyoma amesema walifanya hivyo kuwadhibiti baadhi ya madereva wa bajaji na bodaboda waliokuwa wakivusha watu eneo hilo.

Habari zinazohusiana na hii

“Wananchi sijui wana shida gani, hivi hawawezi kufikiria mpaka wasubiri polisi wawakamate, tunajihami kwa ajili ya wananchi ili yasije kutokea madhara" amesema.

Amesema kutumia barabara hiyo ikiwa imefungwa kwa chombo chochote cha usafiri ni kuhatarisha maisha kwa sababu hakuna anayejua hali ipoje chini kwenye maji na wingi wa maji.

"Tumefungua, lakini kwa kipindi hiki cha mvua tunaangalia mwenendo wake, hatutasita kuchukua hatua iwapo hali itabadilika, iwapo tutafunga wananchi wasilazimishe kupita kwa usalama wao," amesema Kamanda Mwakyoma.



Chanzo: mwananchi.co.tz