Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bakwata yataka watendaji Serikali ya Tanzania kutoka haki bila ubaguzi

Tue, 13 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) limewataka watendaji wa Serikali kuendelea kutoa haki kwa wananchi bila kujali itikadi za kisiasa na kiuchumi.

Akitoa salama za Bakwata, katibu mkuu wa baraza hilo Mwalimu Nuhu Jabil Mruma amesema utendaji wa haki ndio msingi bora wa kuimarisha amani na utulivu ndani ya nchi.

Kiongozi huyo amezungumza hayo leo Jumatatu Agosti 12, 2019  wakati wa Swala ya Eid-El-Adh’aa na Baraza la Eid kitaifa lililofanyika kwenye viwanja vya msikiti wa Kibadeni, Chanika jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Muruma amesema moja ya mambo yanayosababisha wananchi kukosa imani na Serikali yao ni kwa baadhi ya watendaji kuendekeza maslahi yao binafsi ikiwamo kudai rushwa, kuweka urasimu katika utoaji wa huduma za kijamii, ufisadi na mengine.

“Tunaomba Serikali yetu tukufu kuwachukulia hatua kali baadhi ya watendaji hao na sisi viongozi wa dini tupo tayari kushirikiana na Serikali kwa kutoa elimu kwa waumini wetu juu ya madhara ya matendo hayo,” amesema Mwalimu Muruma.

Ameeleza kuwa ili kuendelea kudumisha amani, viongozi wa dini wanatakiwa kuimarisha kamati za amani katika maeneo mbalimbali nchini na kuzifanya ziwe hai wakati wote.

Habari zinazohusiana na hii

Amewataka Waislamu na Watanzania kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la kupiga kura ili wakati wa uchaguzi wawe na sifa stahiki zitakazowawezesha kuchagua viongozi wenye sifa.

“Tunajua kuwa hivi karibuni tunaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, wananchi wote tunaomba watoe ushirikiano ili siku ya kupiga kura ikifika kusiwe na kikwazo,” amesema Mwalimu Zuberi.

Pia, amewataka Serikali na wadau wengine wa uchaguzi kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati ili kuepuka mianya ya kuharibu shughuli hiyo kwa maslahi binafsi.

“Bakwata linaipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa namna inavyowathamini viongozi wa dini katika ngazi zote, hakika ushirikishwaji huu unawafanya viongozi wa dini kuendelea kufikisha taarifa mbalimbali muhimu kwa jamii,” amesema kiongozi huyo wa Bakwata.

Amewataka viongozi na watendaji wa Serikali ambao hawajatambua viongozi wa dini waanze kuwatambua viongozi hao na kuanza kushirikiana nao kutokana na umuhimu wao kwenye jamii.

Katibu Mkuu huyo wa Bakwata amesema kwa muda mfupi wa baraza hilo limefanikiwa kutengeneza umoja na ushirikiano baina ya taasisi zote za Kiislamu Tanzania.

“Matokeo yake hakuna vurugu za kidini wala maandamano yasiyo ya lazima, pia tumeweza kuimarisha uhusiano mwema na dini mbalimbali tukiweka utengamano kitaifa uliosababisha utulivu na amani nchini,” amesema.

Kuhusu malezi ya watoto, Mwalimu Muruma amesema Bakwata inasisitiza wazazi kuwalea watoto wao katika misingi ya maadili kwa sababu chimbuko la tabia njema hutokana na malezi ya familia.

Aidha amesema wanaendelea kutambua na kusajili misikiti na madrasa shughuli ambayo ni endelevu na muhimu.

Amesema mpaka sasa Misikiti iliyosajiliwa ni 513, Madrasa 475, Maimamu wa misikiti 348, walimu wa madrasa 692 na wafungishaji ndoa 1904.

Aidha amesema Bakwata inaelekea kwenye kipindi cha uchaguzi wa viongozi kuanzia kwenye misikiti ya mitaa na kwamba, kila Mwislamu atakuwa na haki ya  kuchaguliwa kuongoza.

Chanzo: mwananchi.co.tz