Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bakwata yaomba kesi za mashehe ziharakishwe

4371d907860e3fe9c4498931dbb76f6c.jpeg Bakwata yaomba kesi za mashehe ziharakishwe

Sun, 16 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limeomba kuharakishwa kwa uchunguzi wa kesi inayowakabili mashehe wanane kwa kile kilichoelezwa kuwa imekaa muda mrefu.

Ombi hilo la Bakwata limetolewa na Katibu wa baraza hilo, Nuhu Mruma katika risala yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan jana kwenye Baraza la Idd lililofanyika kitaifa jana Dar es Salaam.

Mruma alisema Bakwata inaunga mkono jitihada za serikali katika kupigania haki, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na demokrasia . Hata hivyo alisema kuna mazingira ya haki kutotendeka.

“Bakwata inaomba uchunguzi wa kesi inayowakabili Mashehe hawa uharakishwe kwa kuwa wamekaa muda mrefu wakiendelea kutaabika gerezani”alisema Mruma.

Mashehe hao wanaokabiliwa na mashtaka ya kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo, walifikishwa mahakamani mwaka 2015.

Pia Bakwata kupitia risala hiyo imeunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kukabili ugonjwa wa covid 19 unaoambukizwa na virusi vya corona hasa kwa hatua yake ya kuunda kamati ya kufuatilia ugonjwa huo.

Pia Bakwata imeunga mkono falsafa ya uchumi hasa kwa hatua ya serikali ya kuwasihi wananchi kujitambua na kubadilika kifikra hasa kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea kuwa na nchi yenye uchumi bora.

Alisema,“Taifa likiwa na uchumi bora, basi hata taasisi zake zinakuwa ni bora na zenye kujielewa hasa katika kushirikiana na serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo.”

Alisema Bakwata itaendelea kusisitiza suala zima la amani kwa kuwa hakuna maendeleo bila ya amani na kuwa Waislamu wataendelea kushirikiana na watanzania wote kwa ujumla kudumisha amani na utulivu wa nchi.

Shehe Mkuu, Mufti Abubakari Zuberi katika hotuba yake alimuomba Rais Samia kusaidia kuondolewa kwa kodi kwenye tende kuondoa changamoto wanayokumbana nayo waumini wa dini ya kiislamu ya ugumu wa kupata bidhaa hiyo kutokana na bei wakati wa mfungo.

Alisema,” Tende na mfungo huenda sambamba yaani kwa waislamu wakati wa mfungo inatakiwa wakati wa kufuturu kuanza kwa kula tende ndiyo vyakula vingine vifuate, lakini imekuwa ngumu kwa baadhi ya waumini kwa kuwa tende zimekuwa bei na hiyo inatokana na kutozwa kodi ziingiapo nchini.”

Wakati huo huo alishauri jamii kuzingatia hadhari dhidi ya corona hasa kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono, kukaa kwa umbali.

Alisema, waislamu wataendeleza amani na utulivu kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu viongozi, kukataa dharau na kuzingatia maelekezo husika kutoka kwa wenye mamlaka.

Alitoa mwito pia kwa Watanzania kuendelea kuishi maisha ya amani na utulivu huku akiwaombea viongozi wote wa serikali baraka waendelee kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, pia amewataka waislamu kuendelea kuishi maisha kama waliyokuwa wakiyaishi wakati wa mfungo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz