Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bakwata wamshukuru Rais Magufuli baada ya kurejeshewa shamba alilouziwa mwekezaji

Wed, 24 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kilimanjaro, limekabidhiwa rasmi shamba ekari 19 alizokuwa ameuziwa ‘kinyamela’ mwekezaji.

Bakwata limempongeza Rais John Magufuli kwa kusaidia kurejeshewa shamba hilo.

Shamba hilo, lililopo kijiji cha Kimashuku aliuziwa mwekezaji huyo, Navitej Mudher Charising kiasi cha Sh150 milioni na aliyekuwa katibu wa Bakwata mkoa wa Kilimanjaro, Rashid Mallya mwaka 2013.

Kaimu Katibu Mkuu wa Bakwata Mkoa wa Kilimanjaro, Awadhi Lema  akizungumza katika kikao baina ya  viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Hai na viongozi wa Bakwata mkoa wa Kilimanjaro leo Jumanne Oktoba 23,2018 amesema mwekezaji huyo amekabidhi nyaraka zote za umiliki wa shamba.

Amesema kutokana na uamuzi huo wa mwekezaji, wanampongeza sana Rais John Magufuli na Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kuingilia kati mgogoro huo wa muda mrefu na kuupatia ufumbuzi.

“Tunamshukuru sana Rais wetu, John Magufuli kwa kusaidia kupatikana haki yetu na wasaidizi wote akiwepo Mkuu wetu wa wilaya, Lengai Ole Sabaya,” amesema

Akizungumza baada ya maelezo hayo, Sabaya amesema uamuzi wa kurejeshwa shamba hilo mikononi mwa Bakwata ulitolewa na Rais John Magufuli, baada ya kupokea maombi kushughulikiwa suala hilo kutoka kwa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zuberi .

“Kutokana maombi hayo ya Muft,i vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama vilianza kufuatilia suala hili na baada ya kujiridhisha kuwa, mmiliki halali wa shamba hili ni Bakwata ndipo Rais alinituma nije kwenu kuwarejeshea shamba letu,” amesema.

 Hata hivyo, aliutaka uongozi wa Bakwata kuhakikisha sasa unalitumia shamba hilo kwa maslahi ya mapana ya Waislam wote, kwa kuendeleza kilimo, ama kufanya shughuli nyingine.

“Kikubwa ambacho tunawaomba ni kuhakikisha shamba hili linaendelezwa na halibaki pori kwani ndio nia ya Serikali,” amesema

Lengai ameagiza halmashauri ya wilaya hiyo, kuhakikisha wanashughulikia haraka Bakwata ipate hati miliki ya eneo hilo.

Mkurugenzi wa ya  halmashauri ya Hai, Yohana Sintoo ameahidi kuhakikisha ndani ya muda mfupi hati miliki inapatikana.

“Tutashughulikia mpate hati ndani ya muda mfupi na kama mna maeneo mengine ambayo hayana hati mnaweza kutuletea kushughulikia kwa pamoja,” amesema.

Akizungumza baada ya maelekezo hayo, Kaimu Sheikh wa Mkoa Kilimanjaro, Mlewa Shabani ameahidi ardhi hiyo kutumika kama ilivyokusudiwa.

Hivi karibuni, mkuu huyo wa wilaya akiwa na ujumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Hai, walitembelea shamba hilo lenye mgogoro na kumwagiza mwekezaji huyo ambaye alikuwa amelima mbogamboga kulikabidhi kwa Bakwata.

Hata hivyo, mwekezaji huyo alikubali uamuzi huo licha ya kudai alinunua kwa Mallya na alifuata taratibu zote.

Chanzo: mwananchi.co.tz