Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BAKWATA yafanya mabadiliko makubwa ya kupata viongozi nchi nzima

5917 SHEIKH ABUBAKAR ALLY TZW

Fri, 6 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

ILI kuziba mianya yote ya ufi sadi wa mali za Waislamu, Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) limefanya marekebisho makubwa ya Katiba yake kwa kuingiza kipengele kinachoagiza kutoruhusiwa kuuzwa kwa mali yoyote iliyo chini ya Wakfu wa dini hiyo.

Ukiondoa mabadiliko hayo muhimu katika uhai wa baraza hilo lililotimiza miaka 50 tangu kuundwa kwake, Katiba hiyo pia imefanyiwa marekebisho makubwa na muhimu ambayo yanafuta mfumo wa awali wa Mashehe wa Mikoa, Wilaya, Kata na Maimamu wa Misikiti kupatikana kwa njia ya uchaguzi. Katika hatua nyingine, Tume iliyoundwa na Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeiry, imemaliza kazi yake na kukabidhi ripoti yake kwa Mufti ambaye naye tayari ameiwasilisha kwa Rais John Magufuli ili kutafuta nguvu za kisheria za kufikia ufumbuzi.

Mabadiliko hayo makubwa ambayo yanakwenda sambamba na falsafa mpya ya Bakwata Mpya, Jitambue, Badilika ni uamuzi uliofikiwa wakati wa Mkutano Mkuu wa baraza hilo uliofanyika Machi 31 na Aprili 1, mwaka huu, mjini Dodoma. Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Shehe Khamis Mataka akizungumza na wahariri na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alisema katika marekebisho yaliyofanywa ili kulinda mali za Waislamu kutouzwa tena kama ilivyokuwa nyuma, kimeingizwa kipengele mahususi ndani ya Katiba kuzuia.

“Sasa suala la mali za Wakfu zimewekewa kipengele maalumu ndani ya Katiba na hivyo zinalindwa Kikatiba. Haitawezekana tena kutokea mtu au kikundi cha watu watakaoweza kuuza mali hizo kama ilivyokuwa zamani,” alisema Shehe Mataka. Akizungumzia marekebisho ya Katiba yaliyofuta Mashehe wa Mikoa, Wilaya, Kata na Maimamu kupatikana kwa njia ya uchaguzi, Shehe Mataka alisema mfumo mpya uliopitishwa na Mkutano huo Mkuu, utafanyika kuanzia sasa viongozi hao wa dini kupatikana kupitia uteuzi. Alisema Mashehe wa Mikoa na Mashehe wa Wilaya sasa watateuliwa na wajumbe wa Baraza la Ulamaa la Bakwata Taifa ambao wao hupatikana kwa kuteuliwa na Mufti.

Kwa upande wa Mashehe wa Kata, alisema kwa utaratibu wa sasa watapatikana kwa kuteuliwa na Bazara la Mashehe la Mkoa, wakati Maimamu wa Misikiti sasa watateuliwa na Baraza la Mashehe wa Wilaya. Mabadiliko mengine makubwa ni katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato ili kudhibiti mapato ya taasisi hiyo, ambapo Shehe Mataka alisema sasa kutakuwa na mfumo mmoja wa ukusanyaji kuanzia ngazi ya Msikiti, Kata, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.

Alisema chini ya mfumo huo watatafutwa watu wenye taaluma ya Uhasibu ili kusimamia jukumu hilo na kutaaundwa mfumo maalumu wa ukaguzi wa ndani ili kuangalia namna mapato yanavyokusanywa na kutumika na alitoa mwito kwa waumini wa dini ya Kiislamu wenye taaluma ya Uhasibu kujitokeza ili kufanya kazi hiyo kwa kujitolea. Alisema: “Kwa vile kwa sasa hatuna fedha za kulipa mishahara chini ya mfumo huu mpya, hivyo wale watakaojitokeza watakuwa wanafanya kazi chini ya mfumo wa kujitolea. Lengo ni kuhakikisha baadaye tunaweka mfumo wa kukusanya mapato kielektroniki.”

Kuhusu ripoti ya Tume maalumu iliyoundwa na Mufti Zubeir ili kuchunguza uuzwaji wa mali za Waislamu, Shehe Mataka alisema tayari imemaliza kazi hiyo na kuiwasilisha kwa Mufti Zubeir ambaye naye ameiwasilisha kwa Rais Magufuli ili kupata nguvu za kimamlaka za kuipatia ufumbuzi. “Tayari Mufti ameikabidhi kwa Rais na tayari baadhi ya Mamlaka za kiserikali ikiwemo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wameanza kufanyia kazi ripoti na mapendekezo ya Tume,” alisema.

Akitoa salamu zake, Mufti Zubeir aliwataka waislamu wote nchini kubadilika na kuwa kitu kimoja na kuhakikisha kila mmoja kwa uwezo wake anasaidia katika kuijenga Bakwata mpya. Alisema wakati Baraza hilo lililoanzishwa mwaka 1968 limetimiza umri wa miaka 50 mwaka huu, mkakati ni kujipanga kufanya mapinduzi makubwa ya uendeshaji wake kwa miaka 50 ijayo, kwa kujikita katika mapinduzi ya kiuchumi, na kukuza maendeleo ya kisekta kama elimu, afya na miundombinu.

Chanzo: habarileo.co.tz