Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma ameeleza ni jukumu la viongozi wa dini kuishauri, kushirikiana na kuiungana na Serikali katika kuiombea nchi na viongozi wake.
Mruma ameyasema hayo leo, Jumatatu Agosti 21, 2023 alipotoa salamu katika hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) iliyofanyika jijini Arusha.
Barza hilo, amesema limekuwa likishirikiana na makanisa mbalimbali katika shughuli zake, katika ile kaulimbiu ya ‘dini mbalimbali umoja na amani’.
"Sisi viongozi wa dini tutaendelea kuiombea nchi yetu na kuendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo," amesema Mruma akimwakilisha Mufti Mkuu wa Tanzania, Mohammed Bin Zubeiry.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema KKKT imechangia mambo mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.
Katika Mkoa wa Arusha, amesema KKKT imefanya kazi kubwa huku akiahidi kuendelea kushirikiana nalo kwa maendeleo ya nchi.