Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu awapasha wanaosaka utajiri

60072 ASKOFU+PIC

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecostal Bible Fellowship Tanzania (PBFCT), Japheth Mapogo amesema hakuna mtu aliyewahi kutajirika duniani kwa kuombewa bila kufanya kazi kwa bidii.

Askofu Mapogo alitoa kauli hiyo juzi kwenye mahubiri ya ibada ya Jumapili katika kanisa hilo lililopo Dodoma Makulu.

Alisema ili mtu atajirike lazima afanye kazi kwa bidii si kwa kuombewa na kuwekewa mikono na watumishi wa Mungu.

“Hata kama wakikusanyika watumishi wote wa Mungu duniani unaowajua wewe, wakaja wakakuombea kwa kukuwekea mikono ili uwe tajiri hautakuwa hata siku moja, dawa ni kufanya kazi kwa bidii maana Mungu hubariki kazi za mikono yetu,” alisema Askofu Mapogo na kuongeza:

“Kuna baadhi ya watu hawataki kufanya kazi lakini wanataka wabarikiwe kwa kuombewa na watumishi, hii si sahihi, ukitaka kufanikiwa lazima ufanye kazi kwa bidii.”

Aliwataka wanawake wa kanisa hilo kufanya kazi za mikono na kuachana na utegemezi kwa waume zao.

Pia Soma

“Na ndiyo maana tukitangaza michango kanisani mwitikio unakuwa ni mdogo kwa kuwa watu wengi hawafanyi kazi, sasa hizo fedha wanazitoa wapi?” Alihoji.

Alisema maandiko Matakatifu ya Mungu yanawaagiza watu wafanye kazi kwa bidii kwani hata Mungu alifanya kazi siku sita ya saba akapumzika, hivyo lazima kila mtu mwenye afya njema kufanya kazi ili kupitia kazi hiyo Mungu aweze kumbariki na kumpa utajiri.

Naye katibu wa kanisa hilo, Lilian Mushi aliwataka waumini kufanya kazi bila kuchagua kwa kuwa hakuna kazi inayodharaulika kama inaingiza kipato.

Mushi aliwataka waumini wa kanisa hilo kila mmoja kuwa na shughuli ya kiuchumi inayomuingizia kipato hata kama ni kidogo kuliko kukaa bila kufanya kazi.

Manabii, viongozi wa dini

Machi 9, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo aliisihi Serikali kuwa makini na manabii na viongozi wa dini wanaotoa mafundisho potofu na kutumia mahangaiko ya waumini wao ili kujitajirisha.

“Ni lazima Serikali ijue historia ya hao (manabii) wanaoibuka na umiliki wa huduma zao uchunguzwe vizuri. Nafikiri Serikali yetu inalo la kujifunza kwa Serikali ya Rwanda,” alisema Askofu Shoo.

Pia, Askofu Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema kanisa la kweli limepewa wajibu wa kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili si kujitajirisha kwa mali na fedha.

Naye mhadhiri wa vyuo mbalimbali vya dini, Dominic Tarimo alidai wengi wa wachungaji wa madhehebu yanayoibuka kila uchao hawana elimu ya theolojia ya kuwasaidia kuyaongoza.

Chanzo: mwananchi.co.tz