Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu awakemea wateule wa Rais Magufuli

90547 Mkesha Askofu awakemea wateule wa Rais Magufuli

Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Askofu mkuu wa Tanzania Fellowship of Church (TFC), Godfrey Malasi amesema viongozi wanaoshindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya kuleta maendeleo wamegeuka washangiliaji wa kila kitu badala ya wasaidizi wa Rais John Magufuli.

Amesema hatua hiyo inawafanya kumbebesha mzigo kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Hayo yamesemwa katika ibada ya kuliombea taifa iliyofanyika jana usiku Jumanne Desemba 31, 2019 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam uliokuwa umebeba kauli mbiu isemayo ‘Nchi nzima Sauti moja bila Amani hakuna Maendeleo.’

Mbali na kuliombea taifa katika mkesha huo pia maombezi mbalimbali yalifanyika ikiwamo kuwaombea viongozi ili waweze kufanya kazi kwa weledi, nidhamu kwa watumishi wa umma, kuvunja matendo yanayoenda kinyume na matakwa ya nchi ikiwemo Ushoga, usagaji.

Akizungumza katika mkesha huo, Malasi alisema Rais Magufuli anapochagua wasaidizi hutegemea kuona kazi zinarahisishwa jambo ambalo linakuwa kinyume kwa baadhi ya wateule.

“Imefika mahali tumebaki kushangilia wakati tunamtwika mzigo huo peke yake, hatuwezi kukaa afanye kila kitu kwa ajili ya nchi nzima bali kila mmoja amsaidie isiwe kama wamemuachia mchezo wote acheze mwenyewe,”

“Yapo mambo mengi tunayopasa kufanya kila mmoja wetu ili kumsaidia kwa kufuata maelekezo yake,” alisema Malasi

Pia, uelewa mdogo wa wananchi katika kusaidia kusukuma kasi ya uchumi wa viwanda imekuwa ni changamoto katika kuongeza kasi ya maendeleo kwani wamegeuka kuwa wachuuzi badala ya wazalishaji wa bidhaa hizo

Alisema kauli mbiu ya Tanzania ya viwanda inamtaka kila mmoja kushiriki kikamilifu na siyo kuzurura mtaani ukiuza vifaa vya urembo badala ya kwenda kulima na kuzaisha mazao.

“Neno la Mungu linasema asiyefanya kazi na asile, ukimuona mtu ananing’iniza ushaga mwambie aende vijiji akalime tupate mazao sababu mambo ya kuning’iniza shanga haliwezi kuleta mabadiliko yoyote kwenye Tanzania ya viwanda,” alisema 

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkesha huo, Innocent Bashungwa alisema azma ya Serikali ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kunufaisha Watanzania na ili kufanikisha hilo mikakati ya kuweka miundombinu itakayosaidia suala hilo inaendelea kujengwa.

“Siyo kama awali hazikuwapo bali zilikuwa zikitumika katika kuwanufaisha watu wachache badala ya wengi waliopo hivyo sasa tunataka kuona jinsi gani Kilimo, utalii vikiwanufaisha wengi na hii ni baada ya kufungamanisha rasilimali hizi kupitia uwekezaji mkubwa wa kujenga miundombinu,” alisema Bashungwa

Alisema tayari maboresho yamefanyika Brela, TBS na EPZA huku akibainisha kuwa tayari fidia imeshalipwa kwa ajili ya kujenga eneo maalumu la uchumi Kurasini litakalotumika kuchakata mazao kabla ya kupelekwa nje ya nchi.

“Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 22.5 tumeshaliandaa, tutajenga miundombinu ya kisasa ili kuhakikisha tunachakata mazao yetu na kutengeneza ajira za akina mama na vijana na ili kuboresha uchumi wa nchi,” alisema Bashungwa

Chanzo: mwananchi.co.tz