Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu atoa ujumbe kwa wazazi kuhusu malezi kwa watoto

33444 SKOFU+PIC Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kuporomoka kwa maadili na kuongezeka kwa watoto wa mitaani kumetokana na wazazi kushindwa kutimiza jukumu lao la malezi bora kwa watoto pamoja na ndoa nyingi kuvunjika na hivyo watoto kulelewa na mzazi mmoja. Hayo yalisemwa leo Desemba 25, 2018 na Askofu wa Kanisa na Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, Jacob Ole Mameo wakati akitoa salam za Sikukuu ya Krismasi mara baada ya kuendesha ibada katika kanisa la Bungo Manispaa ya Morogoro. Askofu Mameo amesema wazazi wengi kwa sasa wamekuwa wakishindwa kutimiza jukumu lao la malezi ya watoto badala yake wamekuwa wakiwaachia jukumu hilo wasichana wa kazi za ndani na wengine kuthubutu kuwapeleka shule za bweni ili kukwepa malezi ya watoto wao. Ametoa rai kama wazazi hawatawajibika katika kuwalea vyema watoto wao Taifa la baadaye litaingia katika matatizo makubwa kwani litaendeshwa na watu wasiokuwa na maadili. Amewataka waumini wa Kikristo pamoja na Taifa kwa ujumla kutambua na kuthamini haki za mtoto ikiwa ni pamoja na kupelekwa shule ili kuweza kuzalisha taifa la baadaye lenye wasomi na wataalamu badala ya kuwaacha watoto waige tabia na tamaduni za mataifa mengine. Miongoni mwa waliohudhuria ibada ya Krismasi katika kanisa hilo ni pamoja na mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo ambaye amesema jamii inapaswa kusaidiana na Serikali katika kuondoa tatizo la watoto wa mitaani na kusimamia maadili ya watoto katika maeneo yao. Chonjo amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatelekeza watoto kwa bibi zao bila hata kuwahudumia na hivyo kusababisha watoto hao kuingia mtaani kuombaomba, kufanyiwa vitendo vya ukatili na wengine kutumikishwa kazi ngumu na zisizokuwa na staha jambo ambalo ni kosa kisheria. Aidha mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya amesisitiza suala la amani kwani kama taifa halitakuwa na amani hakuna maendeleo yatakayopatikana. Naye kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Wilbrod Mutafungwa ambaye naye alihudhuria ibada hiyo amesema jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimeendelea kusimamia na kuimarisha ulinzi na kwamba mkesha wa Krismasi katika makanisa yote ulimalizika salama.

Chanzo: mwananchi.co.tz