Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu ataka amani ya nchi ilindwe na kudumishwa

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma mkoani Mara, Michael Msonganzila amewaasa waumini wa jimbo hilo na Watanzania kwa ujumla kudumisha amani na upendo ili kulinda amani ya nchi.

Askofu Msonganzila ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari mosi 2019 wakati wa misa takatifu ya kumshukuru Mungu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mama wa Mungu mjini Musoma.

"Migogoro midogo midogo isiwafanye mvunje amani tuliyonayo tangu uhuru na kusababisha machafuko, kila mmoja wetu ana wajibu wa kuilinda nchi yetu na kukataa dalili zozote za uvunjifu wa amani," amesema Askofu Msonganzila.

Amewataka pia viongozi wa vyama na Serikali kuhakikisha wanahubiri amani kila mara, kwani maendeleo ya nchi yaliyopo yanatokana na uwepo wa hali nzuri ya utulivu na kuvumiliana katika hali zote iwe kidini, kisiasa na hata kiuchumi katika nchi yetu, hivyo tusikubali wala kuruhusu amani tuliyonayo ikapotea.

Amewakumbusha wazazi na walezi ndani ya familia kuhakikisha nyumba zao zinakuwa na amani, upendo na mshikamano ili kujipatia maendeleo na hivyo kuondokana na umasikini, kwani matatizo ndani ya familia nyingi yamekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani na kusababisha familia kufarakana na hata kutengana kabisa.

Amewaomba wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa na umoja katika kupambana na vita ya umasikini, maradhi na ujinga ili tunapokimbizana na sera ya nchi ya uchumi wa viwanda kila mmoja aweze kuona manufaa katika kujikwamua kimaisha.



Chanzo: mwananchi.co.tz