Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu atahadharisha wenye mamlaka nchini

45726 Pic+askofu Askofu atahadharisha wenye mamlaka nchini

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Songea. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea, Damian Dallu amewataka watu waliopewa mamlaka kutowanyanyasa wanaowaongoza, pamoja na kutoigombanisha Serikali na makanisa kwa kuvifungia vituo vinavyohudumia watoto yatima kwa kutaka vilipe kodi ya biashara wakati hakuna biashara inayofanyika.

Askofu Dallu alitoa rai hiyo kwenye mahuburi yake ya Misa ya Jumatano ya Majivu wiki hii iliyofanyikia katika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea.

Aliwataka watu wenye mamlaka kuacha kuvifungia au kuvitishia vituo vya kulelea watoto yatima, wajane na watu wenye uhitaji (maskini) vinavyomilikiwa na makanisa kwa kudai ni biashara wakati si biashara.

“Wakivifungia vituo hivyo ni sawa na kufungia uhuru wa kuabudu kwa watu ambao wanahudumiwa na vituo hivyo, kuna watu wanajitolea kuhudumia vituo hivyo kwa kutoa zawadi na kuwasaidia maskini kwa moyo lakini mamlaka huwapeleka hadi mahakamani.”

“Vituo vingi vinatunzwa na watawa wamisionari, hivyo wakiamua kuvifungia ni sawa, ila viongozi wa dini tutamuachia Mungu kwani ndiye anayejua umuhimu wa makanisa kusaidia wahitaji hao na tunapotoa misaada hiyo si kwamba tunaisaidia Serikali bali tunatekeleza wajibu wa kanisa na huo ni wito wetu,” alisema.

Askofu Dallu aliwaonya viongozi waliopewa mamlaka ya kuongoza watu kuacha kufanya kazi kwa kunyanyasa wananchi na kuwachonganisha na Serikali yao na kusema kama wanaogopa kutumbuliwa safari hii watatobolewa.

Aidha, askofu huyo aliwataka waumini wa kanisa hilo kutumia mfungo kwa Kwaresma kusali, kutubu na kuwajali watu wenye uhitaji na kuacha tabia ya kutoa zawadi au misaada kwa kujionyesha katika jamii kwa kutumia vyombo vya habari ili kujulikana wamesaidia kitu katika vituo vya kulelea wahitaji bali wawe wanatoa kwa siri kwani ni sadaka na pia ni moja ya ibada.



Chanzo: mwananchi.co.tz