Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu asimikwa, awataka Watanzania kupinga ushoga

33108 Askofu+pic Askofu Mteule wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Mwanza, Philipo Magwano

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Askofu Mteule wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Mwanza, Philipo Magwano amesema inahitajika nguvu ya pamoja kwa viongozi wa dini kupinga asasi zinazotetea na kuhamasisha suala la ushoga nchini.

Pia, amewataka Watanzania kutoogopa kunyimwa misaada kutoka nchi zilizoendelea au kwa wahisani kwa sharti la kukubaliana mambo yanayoleta chukizo mbele za Mungu na yale ambayo ni kinyume na utamaduni wa Tanzania.

Askofu Magwano ameyasema hayo kwenye hotuba yake leo Jumapili Desemba 23, 2018 jijini Mwanza katika sherehe za kumuwekea wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa AICT Dayosisi ya Mwanza ambapo amesema jamii inaporomoka kwa maadili.

“Nipo kinyume na asasi zinazotetea ushoga, tunahitaji kurejesha maadili kwenye jamii kwa vijana wanaotumia dawa za kulevya, makahaba, walevi, mashoga na wauaji, wote hawa wanahitaji habari njema,” amesema Askofu Magwano saa chache baada ya kusimikwa

Pia, amesema viongozi wa dini wanatakiwa kujiepusha kutoa habari za uchonganishi, uchochezi kati ya tabaka la chini na la juu, mifarakano bali mahubiri yao yalenge katika upatanishi wa jamii na kukemea vitendo vya mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi.

Amesema kanisa hilo linatambua jitihada za Serikali hivyo watakuwa bega kwa bega kushiriki kulijenga taifa hasa katika kipindi hiki cha kufikia uchumi wa kati.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT, Musa Magwesela amesema watumishi wote kwenye taasisi za dini na umma wanatakiwa kutokuwa na aibu na kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na ujasiri mkubwa.

Amesema mambo yanayowaangusha watumishi wengi ni ulevi, uzinzi na wizi ambayo pia yanamchukiza Mungu katika utume uliotukuka.

 

Akizungumza katika sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini maana inatambua mchango mkubwa katika jamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya na kuijenga jamii katika maadili.

Hata hivyo, amewataka viongozi hao wa dini kuendelea kuhimiza, utulivu, nidhamu na amani kwa waumini maana ndio msingi wa maendeleo yoyote ya binadamu.

“Kupitia huduma za kiroho na kimwili mnazotoa kwa waumini, bila shaka mnawakumbusha na kuwasaidia waumini kufanya kazi, kuondokana na umasikini, maradhi na ujinga,” amesema Mongella huku akilipongeza kanisa hilo kuwa na vituo vingi na hospitali kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa Watanzania.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz