Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu akemea ushoga

Sun, 11 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bukoba. Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Desiderius Rwoma amekemea vitendo vya ushoga huku akishauri wanaume wanaoanguka katika dhambi hiyo wasitengwe bali wasaidiwe kunyeshwa ubaya wa vitendo vyao.

Akihubiri jana wakati wa maadhimisho ya siku ya wanaume wa Jimbo hilo, Askofu Rwoma alisema vitendo hivyo ni aibu na laana ingawa wanaojihusisha wanastahili kupata huduma ya matibabu na msaada wa kisaikolojia.

“Hii ni dhambi kama ilivyo dhambi nyingine, kumvumilia mkosefu siyo kwamba unamuunga mkono. Aliye na tabia hii asaidiwe na kuonyeshwa ubaya wa kile anachokifanya hizi ni fikra potofu kuwa kila kinachofanyika Ulaya ni kizuri,’’ alisema Askofu Rwoma.

Pia, Askofu Rwoma alipendekeza kutungwa haraka kwa sheria za kudhibiti vitendo vya ushoga akisema kuigiza kila kitu kutoka nje ya nchi, matokeo yake yanakuwa siyo mazuri kama inavyotokea kwa ushoga hivi sasa.

Akisisitiza umuhimu wa siku hiyo, Askofu huyo alisema ni vyema wanaume na wanawake wakashindana kwa mambo mema siyo kwa nia ya kudhoofishana kwa kuwa makundi hayo yana nguvu na sauti kubwa kwenye jamii.

Aliwataka wanaume wa Jimbo hilo kujiimarisha kupitia jumuiya ndogondogo huku wakijenga msingi imara kwa watoto wao kupitia mafundisho ya dini na imani, ili baadaye waweze kuchukua majukumu ya familia.

Tamko la Serikali

Baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza kampeni ya kutokomeza vitendo vya ushoga na usagaji jijini hapa, Serikali ilitoa tamko la kujitenga na kauli hiyo.

Licha ya Serikali kusema haihusiki na suala hilo, hata wadau mbalimbali walipinga mfumo wa uendeshaji wa kampeni hiyo wakieleza kuwa inadhalilisha.

Oktoba 31, katika mkutano na waandishi wa habari, Makonda alitangaza kampeni ya kupambana na vitendo hivyo katika mkoa wake, huku akiunda kamati ya watu 15 kwa ajili hiyo.

“Serikali ya Tanzania ingependa kufafanua kwamba hayo ni mawazo yake (Makonda) na si msimamo wa Serikali,” ilisema sehemu ya taarifa ya wizara hiyo.

Serikali ilisema kuwa itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo imesaini na kuridhia.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola juzi alitoa msimamo wa Serikali kuhusu vitendo vya ushoga akipinga vikali vitendo hivyo na kuwa havitaruhusiwa nchini kwa kuwa ni kinyume cha maadili na utamaduni wa Mtanzania.

Lugola alisema vitendo hivyo haviruhusiwi na havitaruhusiwa huku akiwaonya wanaojihusisha navyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz