Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu aishauri Serikali kuhusu uharibifu wa mazingira

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora, Dk Elias Chakupewa ameiomba Serikali kupunguza gharama za nishati ya  gesi ili wananchi waimudu na kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni yanayoharibu mazingira.

Dk Chakupewa alitoa kauli hiyo, leo Jumatatu Februari 25, 2019 wakati wa kongamano la kujadili hali ya mazingira ya mkoa wa Tabora lenye kauli mbiu ‘utunzaji wa mazingira kwa maendeleo ya Tabora’.

Kongamano hilo, limehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mwita Waitara, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatino Kanyasu.

Amesema uharibifu wa mazingira unasababishwa na shughuli mbalimbali ikiwemo ukataji wa miti inayotumika katika kuni na mkaa ambao kwa kiasi kikubwa unatumika Dar es Salaam.

“Serikali ni vyema ikapunguza gharama ya nishati ya gesi ili watu hasa wa mkoa wamudu kununua ili kuondokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa,” amesema Dk Chakupewa.

Mbali na hilo, kiongozi huyo wa dini ameshauri pia uongozi wa mkoa huo kuyahamisha madampo yaliyopo katika mji ili kuondoa mlundikano wa taka.

Kwa upande wake, mratibu wa wajasiriamali mkoani humo Ashura Shaaban aliwaomba wana Tabora kuungana na Samia katika jitihada za kulinda, kuhifadhi na kutunza mazingira.



Chanzo: mwananchi.co.tz