Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu aipongeza Serikali, ataka isiwabague wananchi

33267 Pic+askofu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Isaac Amani

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Isaac Amani amepongeza juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za jamii zikiwemo afya, maji na miundombinu ya usafiri.

Askofu huyo amesema hayo leo Jumatatu Desemba 24, 2018 katika ibada ya Umoja wa Makanisa ya Kikristo jijini hapa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku akisisitiza kuwa mipango ya maendeleo inapaswa kuwa shirikishi kwa kuwafikia watu wote bila kubagua.

Amesema kwa mujibu wa biblia binadamu ameandikiwa kati ya miaka 70 hadi 80 hivyo haipaswi kuwa ya hofu, taabu na mashaka bali iliyojaa amani na furaha huku kila mtu akifanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

"Nitoe wito kwa Serikali kuwasikiliza wananchi kupitia viongozi waliochaguliwa hasa wabunge ili kujenga taifa imara na lenye mshikamano katika kupiga vita uonevu, dhuluma na dawa za kulevya," amesema Askofu Amani. 

Naye mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema amani na utulivu  vimechangiwa na ushirikiano uliopo kati ya Serikali, viongozi wa dini na wananchi wanaomwabudu Mungu kupitia imani zao.

Ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kutoa ushauri kwa Serikali wakati wowote wanapoona inafaa kwani ustawi wa nchi unategemea michango ya watu mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo jijini hapa, Dk Stanley Hotay amekemea tabia inayoenea kwa kasi nchini ya michezo ya kubahatisha inayohamasisha kutofanya kazi bali kutegemea utajiri wa haraka. 

Amepongeza juhudi za mkoa kuinua kiwango cha elimu kwa kushika nafasi ya tatu kitaifa kwenye matokeo ya darasa la saba yaliyotolewa mwaka huu.

Dk Hotay aliwashauri wananchi kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa amani na utulivu kwa kuzingatia matumizi mazuri ya fedha.



Chanzo: mwananchi.co.tz