Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Shoo ataka wananchi kufuata maelekezo ya Serikali kuhusu corona

102217 Pic+shoo Askofu Shoo ataka wananchi kufuata maelekezo ya Serikali kuhusu corona

Mon, 13 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk Fredrick Shoo amewataka wananchi kuchukua tahadhari zote na kufuata maelekezo  yanayoelekezwa na Serikali juu ya kujilinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona na kila mmoja kutambua anao wajibu wa kujilinda na kuwalinda wengine.

Mbali na hilo, Dk Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo amewataka wananchi kumgeukia na kumtegemea Mungu katika kipindi hiki kigumu cha janga la virusi vya corona, kwa kuwa kwa akili, nguvu na uwezo wa binadamu wenyewe, hawataweza kupambana na janga hilo.

Shoo ameyasema hayo leo Jumapili, Aprili 12, 2020, wakati akihubiri kwenye ibada ya Pasaka, katika usharika wa Moshi mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo, ambapo amesema ni wakati wa kila mmoja kuomba na kumuita Mungu kama gamilia, kanisa na Taifa ili aweze kuliondosha janga la corona, ambalo limekuwa tishio duniani kote.

“Tuchukue tahadhari zote na kufuata maelekezo yote, lakini tusiache kumtazama huyu Yesu aliye nguvu na tumaini letu lililo kuu kuliko yote, tumuombe sasa huyu Yesu mfufuka, aturejeshee tena amani, tumaini, atupe uhai na kutukingia hatari zote, hata janga hili la corona, ambalo limeachilia hofu na huzuni duniani," amesema Dk Shoo.

“Yesu kristo anasema tusiogope. Wapendwa neno hili likawe ujumbe mkuu wa pasaka na nguvu yetu, gonjwa hili linatisha, watu wamejawa hofu sana, lakini hofu yetu isitupe kutaharuki na kukosa amani ya ndani bali amani yetu ikawe ni tunaye Yesu mfufuka, ambaye ni nuweza wa yote."

“Tutoke hapa tukiwaambia watu corona ipo tujihadhari lakini Yesu Kristo yupo, ambaye ni mshindi wa kifo na mauti, tuendelee kumuomba na kumuita Mungu maana yeye mwenyewe aliahidi, tukimuita ataitika na kutuonyesha mambo makubwa na magumu tusiyoyajua."

Dk Shoo amesema wananchi wote wakiungana pamoja kuchukua tahadhari  na kuzingatia maagizo yanayotolewa katika kuzuia virusi vya corona kuenea na kuomba kwa pamoja Mungu atasikia na kuiponya nchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz