Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Shoo akemea wanaotumia vibaya madaraka

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Askofu mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Glorius Shoo amesema nchini Tanzania kwa sasa kuna wimbi la baadhi ya Wakristo kutukuza fedha na ulevi, baadhi ya waliopewa madaraka wanayatumia vibaya kuwanyanyasa na kuwaonea wengine.

Askofu Shoo ambaye sasa anahudumu kama mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kilimanjaro International Christian Center (KICC) la mjini Moshi amesema hayo wakati akitoa salamu za Krismasi na mwaka mpya leo Jumanne Desemba 25,2018.

“Siku hizi baadhi yetu badala ya kumtukuza Mungu tunawatukuza binadamu. Kunafanyika maonyesho ya fedha, ufahari na karamu za ulevi na ulafi. Mungu hatukuzwi,” amesema.

“Tumeshuhudia waliopaswa kuwa mfano wa kuigwa kama viongozi wa kiroho wakijitukuza badala ya kumtukuza Mungu. Tunashuhudia watu waliopewa mamlaka wakiyatumia kuwanyanyasa na kuwaonea wengine.”

Ameongeza, “Kama tungemtukuza Mungu basi tungekuwa wanyenyekevu kwa kujua kuwa kama sio Mungu kutupa uhai na uwezo basi tusingeweza kuutumia kuwatesa wengine.”

Askofu Shoo amesema hivi sasa badala ya amani katika baadhi ya maeneo unashuhudiwa ukatili, watu kutotendewa haki.

“Ni wakati wa kila aliyekabidhiwa jukumu la utoaji haki kujiuliza kama anachangia amani kwa kutoa haki inayostahili na tena kwa wakati,” amehoji Askofu Shoo.

Askofu huyo amewataka waumini wa kanisa hilo na jamii kutumia siku ya kuzaliwa kwa Yesu kujishusha, kutubu na kutenda haki wakati wote.

 

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz