Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Sangu akemea uchu wa madaraka, rushwa na uonevu

89887 Uchupic Askofu Sangu akemea uchu wa madaraka, rushwa na uonevu

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga. Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Shinyanga nchini Tanzania, Liberatus Sangu amewataka Watanzania kuliombea Taifa liondokane na tatizo la uchu wa madaraka, maonevu na tamaa ya kujilimbikizia mali na utajiri aliyosema ni miongoni mwa sababu zinazochochea machafuko na mauaji katika nchi za mataifa mbalimbali dunia.

Akitoa mahubiri wakati wa ibada ya mkesha wa sikukuu ya Krisimasi iliyofanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano Desemba 25, 2019, Askofu Sangu amesema mifarakano ya uchu wa madaraka katika jamii na baadaye machafuko na adha kwa wananchi wasio na hatia ni matokeo ya watu wengi kukengeuka na kuacha mafundisho mema ya amani zao za dini.

“Vitendo hivi ni matokeo ya kumruhusu shetani kutawala maisha ya mwanadamu. Watu wanaiba, wanashiriki vitendo vya rushwa, wanauana na kudhulumu kwa sababu ya tamaa madaraka, mali na utajiri. Lazima tutumie kuzaliwa kwa Kristo Yesu kukataa dhambi hizi,” amesema

Amesema amani imepungua kuanzia ngazi ya familia na jumuiya ambako kunashuhudiwa mifarakano mengi; kuna unyanyasaji wa wanawake na watoto, kudhulumu wajane na watoto yatima, mambo aliyosema hayaakisi upendo, mshikamano na undugu wa Kikristo ambao pia unafundishwa katika imani zote za dini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya mahubiri hayo, waumini Paulina Mihayo na Julius Maziku wamewaomba Watanzania; kila mmoja kwa nafasi na eneo lake kushiriki kupiga vita viashiria vyote vya uonevu, ubaguzi na dhulumu ya haki na mali kwa sababu vitendo hivyo vikishamiri huondoa amani na utulivu katika jamii.

“Hakuna amani pasipo haki na upendo miongoni mwetu; viongozi wote wa kidini, kijamii na kiserikali watumia nafasi na ushawishi wao kujenga Tanzania yenye amani, upendo na haki kwa wote na makundi yote. Kamwe tusikubali kutenganishwa na tiofauti iwayo yote,” amesema Maziku

Pamoja na matumizi ya sheria kudhibiti rushwa, uonevu na matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za Taifa, Maziku amesisitiza umuhimu kila mmoja kutendewa kwa haki, staha na utu kama njia sahihi ya kuepuka mifarakano na machafuko katika jamii.

Chanzo: mwananchi.co.tz