Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Rwa’ichi atoa neno

9ab213def150f483bd78fb3950bf8e38 Askofu Rwa’ichi atoa neno

Thu, 27 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda-Thaddeus Ruwa'ichi amewahadharisha wanasiasa kutotumia lugha za matusi na kukomoana katika kampeni za Uchaguzi Mkuu bali wawasilishe hoja na vipaumbele safi kwa wananchi.

Aidha amewataka wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge, uwakilishi na urais na Watanzania wote kutambua kuwa fursa ya uchaguzi ni muhimu kwa taifa kwani ndio njia ya kupata uongozi hivyo wasiichezee fursa hiyo.

Ruwa'ichi alitoa hadhari hiyo jana alipozungumza na HabariLEO katika mahojiano maalumu mara baada ya kuongoza Ibada ya Misa Takatifu ya Upadrisho kwa mashemasi Daniel Mayenja na Geoffrey Mtitu wa Shirika la Mtakatifu Augustino waliopata upadri.

Ibada hiyo ilifanyika katika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mavurunza, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Ruwa'ichi alisema uchaguzi ndio fursa pekee taifa limeichagua kama njia ya kupata viongozi, hivyo kampeni zinapoanza, zinapaswa kuzingatia amani na wagombea kuepuka kutumia lugha za matusi na kukomoana, bali kutoa hoja kwa wapigakura.

"Viongozi ni dhamana, uchaguzi si zoezi jepesi kama linavyoonekana, linapaswa kupewa uzito unaostahili. Tunapoanza kampeni wahusika wote wazingatie amani, haki kwa wote. Si kukomoana bali kuibua hoja na kuchambua mambo kwa haki.

Awali akihubiri katika Misa Takatifu, Ruwa'ichi aliwataka mapadri wapya kujua kuwa wameitwa katika kipindi chenye changamoto za utandawazi, hivyo wawe makini ulimwengu asiwaburuze bali wautakase ulimwengu.

Akitoa neno la shukrani, Paroko wa kanisa hilo, Padri Stephano Msomba aliwataka mapadri wapya kutambua kuwa upadri ni huduma kwa watu, hivyo wawe tayari kujitoa kuwahudumia watu.

Imeandikwa na Anastazia Anyimike, Dodoma; John Gagarini, Pwani; John Nditi, Morogoro; Peti Siyame, Sumbawanga; Gloria Tesha, Marten Kayera na Halima Mlacha, Dar.

Chanzo: habarileo.co.tz