ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Beatus Kinyaiya, ametaja sifa saba za viongozi wa kisiasa wanaofaa Tanzania ikiwemo ya kutotoa rushwa na anayejiamini bila kwenda kwa waganga wa kienyeji.
Askofu Mkuu Kinyaiya alitoa kauli hiyo jana wakati akihubiri katika Misa Takatifu ya kubariki Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino, mkoani Dodoma.
Kanisa hilo limefanyiwa ukaribati mkubwa na kupanuliwa. Aliwaomba Watanzania wanapokwenda kupiga kura watazame kiongozi watakayemchagua katika sifa saba kwa kuwa ndoto yao ni kupata viongozi bora na wachapakazi.
Kinyaiya alitaja mambo ambayo wananchi wanapaswa kuangaliwa kwa kiongozi watakaowachagua kuwa ni pamoja na awe na roho ya kimungu. “Awe mcha Mungu, amuogope Mungu, kwa kuwa ukiwa mcha Mungu hutafanya ufisadi dhamira itakusuta, nafsi itakusuta kwa kufanya kitu ambacho hufananii nacho.”alisema.
Alitaja sifa nyingine kuwa awe ni mtu ambaye anaweka Taifa la Tanzania kwanza na akifungua mdomo wake aseme Tanza nia kwanza.
“Katika ukorofi korofi wa kutafuta kura ni rahisi sana kutafuta makando kando yatakayomlinda mtu, kama dini vile mtu anasema nipigie mimi kura kwa sababu ni Mkristo, au kabila moja, ukiona wa hivyo, hafai yaani Taifa moja kwake hamna.”alisema.
Aidha, Kinyaiya aliwasihi wananchi kutafuta kiongozi ambaye atakuwa ni mwajibikaji na awe ni mtu wa kutenda. “Pia awe ni mtu anayetunza tunu za kitanzania na tunu zipo nyingi amani na mshikamano, akija mtu kutueleza vingine hafai.
Awe ni mtu ambaye anatafuta uongozi kwa njia halali na kwa kumwaga sera zinazofaa na zinazotekelezeka.” Alisema pamoja na kuwa yeye hana hulka ya kusifu viongozi, lakini uongozi wa Awamu ya Tano umefanya mengi hivyo akasisitiza haja ya kuchagua viongozi wanaoendeleza mazuri hayo.
Kinyaiya alisema pia kiongozi lazima awe ni mtu anayejiamini, haendi kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli na kupewa dawa ili ashinde.
“Ukifanya hivyo hufai kwa kuwa unatafuta nguvu ya ziada, utakula takataka na utashindwa.”alisema Askofu Mkuu Kinyaiya Alisema ni kiongozi asiwe mtoa rushwa kwa kuwa kama mtu ana uwezo wa kuongoza atashinda bila kuhonga.
“Mbaya zaidi akikupa sahani ya pilau ili umpigie kura thamani yako inakuwa ile sahani ya pilau, anakushusha hadi anakufanya sahani ya pilau au chupa ya bia amekuona hivyo, tusinunuliwe kwa vitu vya hovyo bali tutazame sera na uwezo wa mtu.”alisema.
Askofu Mkuu Kinyaiya alitumia fursa hiyo kuhamisisha Watanzania waliojiandikisha kupiga kura Oktoba 28 wanajitokeze kwa wingi kupiga kura.
“Wakati mwingine tunachanganya mambo tunachukulia yule mtu ni maarufu atapita tu halafu mnakaa nyumbani, mtu huyo A unayesema maarufu ana watu 20 kwa mfano, na B ana watu watano wanaom kubali wakitoka wote kupiga kura anakuwa na watu watano, na huyu A mwenye watu 20 wakitoka watatu kupiga kura atashinda kweli? hivyo timiza wajibu wako kapiga kura.” alisema.
Askofu Mkuu Kinyaiya alimshukuru Rais John Magufuli kwa ujasiri wa kuchangisha upanuzi wa kanisa hilo kwa kuwa waumini wa kanisa hilo waliweka mipango kwa kuchanga lakini hawakufanikiwa kuanza ujenzi.
Alimsisitiza Rais Magufuli aendelee kuwatumbua watendaji wazembe bila kuogopa na kanisa hilo linamuombea aendelee kuongoza Taifa vizuri hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.