Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Mkuu KKKT ataka waumini kuwaepuka manabii wa uongo

Mkuupic Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo

Sun, 14 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amewataka wananchi kuwaepuka manabii wa uongo kwa madai kuwa wamekuwa wakiwalaghai wananchi kwa mafundisho ya uongo sambamba na miujiza ya utajiri kwa maslahi yao binafsi.

Askofu Shoo ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo ametoa rai hiyo leo Jumapili Novemba 14, 2021 katika usharika wa Nronga katika mahubiri yake kwenye ibada ya kumstaafisha kwa heshima mwinjilisti, Donald Lema.

Amesema siku za hivi karibuni kumeibuka wahubiri wengi katika maeneo mbalimbali nchini na hata duniani, wanafundisha mafundisho potofu kwa kuacha kweli ya Mungu, huku wengine wakifikia hatua ya kumdhihaki Mungu jambo ambalo ni hatari.

"Leo kuna mafundisho potofu yanayotolewa na manabii na walimu wa uongo, kwa tamaa zao wenyewe, wanafundisha mambo yasiyo ya kweli, wanahubiri mambo ya kufurahisha watu tu, mambo ya utajiri na mafanikio kwa maslahi yao binafsi."

"Unakuta wanajiita watumishi wa Mungu lakini hawahubiri wala kufundisha habari ya dhambi, hawakemei dhambi wala kuelekeza watu umuhimu wa kutubu na kumrudia Mungu, hii ni hatari sana kwa nyakati za leo. Wanachofanya ni kuwalaghai watu na miujiza ya uongo, na habari za ndoto na maono ya uongo kuhusu mafanikio na utajiri, hawajali kuhusu usalama wa roho za watu," amesema.

Katika ufafanuzi zaidi kiongozi huyo wa kiroho amesema, “leo tumeona anajitokeza mtu anajiita nabii wa manabii, Askofu wa maaskofu anajipa vyeo vyote huku duniani, wanawatia watu sindano za ganzi kwa mafundisho potofu, wanafanya mzaha na neno la Mungu na hata kumdhihaki Mungu, najiuliza unyenyekevu wa watumishi wa Mung umeenda wapi."

"Lakini pia tumeona mtu bila aibu anavaa kanzu la uchungaji, anavaa msalaba lakini kwenye madhabahu yake ameipamba na pombe na wanawake warembo, bila kujua hatupaswi kufanya mzaha na neno la Mungu.Watu wa namna hiyo wanapaswa kukemewa, kwa kuwa wanaweza kufanya hata Taifa, likaingia kwenye hasira ya Mungu. Tusione hayo tukacheka. Neno la Mungu linatuonya leo, kwamba Mungu hadhihakiwi kwa kuwa Mungu, hataacha kuadhibu dhambi na uasi."

Akizungumza katika ibada hiyo, mwinjilisti Donald Lema mbali na kulishukuru kanisa kwa namna lilivyosimama naye kumuunga mkono katika utumishi wake, amesema ataendelea kutumika pale atakapohitajika kuhakikisha kazi ya Mungu inasonga mbele.

Chanzo: mwananchidigital