Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu KKKT avuliwa uchungaji, wachungaji 7 wasimamishwa

8d4d7351886a9f157df85b20ebd1baeb.jpeg Askofu KKKT avuliwa uchungaji, wachungaji 7 wasimamishwa

Wed, 10 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HALMASHAURI Kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (DKM) imewasimamisha kazi wachungaji saba na kumvua uchungaji Askofu wa dayosisi hiyo, Dk Stephen Munga.

Viongozi hao wa kanisa wanakabiliwa na tuhuma ikiwemo ya kushindwa kusimamia mali za dayosisi na kusababisha ubadhirifu wa mamilioni ya fedha.

Taarifa iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mchungaji Godfrey Walalaze ilieleza kuwa uamuzi huo ulifanywa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT-DKM kilichofanyika Oktoba 29, mwaka huu Utondolo wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao hicho kilipitia kwa taarifa ukaguzi wa hesabu za dayosisi kwa kipindi cha mwaka 2019 na mwaka jana.

Novemba 7, mwaka huu, waumini wa dayosisi hiyo walisomewa taarifa fupi kanisani kuhusu uamuzi wa kikao hicho.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Dk Munga ambaye pia alikuwa Mdhamini wa Mali amevuliwa uchungaji na hivyo amepoteza sifa ya kuwa askofu wa dayosisi hiyo.

Iliwataja wachungaji waliosimamishwa kuwa ni Dk Eberhadt Ngugi aliyekuwa Msaidizi wa Askofu na Mdhamini wa Mali, James Mwinuka aliyekuwa Katibu Mkuu na Mdhamini wa Mali, na Dk Anneth Munga aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo-SEKOMU.

Wengine ni Yambazi Mauya aliyekuwa Mkuu wa Jimbo la Tambarare, Paulo Diu aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Kikristo na Elimu, Yohana Titu aliyekuwa Chaplain wa Hospital ya Bombo, na Rodgers Shehumu aliyekuwa Mtunza Hazina wa Jimbo la Tambarare na Hospitali ya Lutindi.

Taarifa ilieleza kuwa sababu nyingine za uamuzi huo ni matumizi mabaya ya madaraka hivyo kusababisha uvunjaji wa Katiba KKKT-DKM, kufanya mambo yanayosababisha migongano na kuchochea vurugu na ukosefu wa amani miongoni mwa waumini wa watumishi wa dayosisi kwa ujumla.

Wakili wa watuhumiwa, Joseph Tadayo jana alikiri kuwa, wateja wake walipokea barua za kusimamishwa kazi za kichungaji katika dayosisi hiyo.

Tadayo alidai wateja wake hawajawahi kuitwa katika kikao kujitetea kuhusu tuhuma zinazowakabili kwa mujibu wa Katiba ya dayosisi hiyo, na kwamba watakuwa tayari kujieleza katika kikao halali na si vinginevyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz