Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu KKKT ataka mwaka 2019 Watanzania wadumishe amani, wasigawanywe

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Askofu Mkuu Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Solomon Masangwa amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani mwaka 2019 na kuacha kugawanyika kutokana na tofauti za kisiasa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari Mosi, 2019 juu ya salamu zake za mwaka mpya 2019, Askofu Masangwa amesema, mwaka 2019 unapaswa kuendelea kuwaunganisha Watanzania wote na kudumisha amani iliyopo na kuepuka migawanyiko ya kisiasa.

Amesema Watanzania bila kujali tofauti zao za kisiasa wanapaswa kushirikiana kufanya shughuli za kimaendeleo, ili kuinua uchumi wa taifa katika kuelekea taifa lenye uchumi wa kati.

"Rais John Magufuli anafanya kazi nzuri katika kuanzisha miradi mbalimbali hivyo ni jukumu letu kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii," alisema.

Akizungumzia hali ya usalama mkoani Arusha, amepongeza vyombo vya dola na wakazi wa Arusha, kwa mshikamano mkubwa uliokuwepo mwaka 2018 na kufanya Arusha kuwa shwari.

"Nina imani kubwa hata mwaka 2019 Arusha itaendelea kuwa ya amani na utulivu na nawapongeza viongozi wenzangu kwa kazi nzuri wanayofanya," alisema.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Arusha, Peter Laizer na Julius Kanangira, wameeleza mwaka 2019, wanatarajia utaendelea kuwa na amani licha ya kuwepo na chaguzi za Serikali za mitaa.

"Amani ndio chimbuko la maendeleo sisi Arusha tunataka amani, vyama vya siasa mwaka huu vifanye chaguzi huru na haki ili kuepusha vurugu," amesema Laizer.

Naye, Kanangira alisema mwaka 2019, wanatarajia miradi iliyoasisiwa na Rais John Magufuli, ikiwepo Reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Arusha itaanza kufanyiwa kazi.

"Tumesikia Rais ameahidi kurejesha Reli ya Dar es Salaam hadi Arusha, tunaomba hili likamilike kwani litaondoa usumbufu wa usafiri wa abiria na mizigo," alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz