Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu KKKT asimulia alivyotimuliwa msibani

KKKTTTT Askofu KKKT asimulia alivyotimuliwa msibani

Sun, 19 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Konde, Dk Edward Mwaikali ambaye yeye na wachungaji wake 85 walitimuliwa kwenye ibada ya mazishi ya mchungaji Japhet Malasusa ameweka wazi kilichotokea.

Tukio hilo ambalo limeibua hisia tofauti kwa wachungaji na waumini wa kanisa hilo baada ya kusambaa kwa taarifa hizo, lilitokea Desemba 15 katika kijiji cha Kiwira eneo la Dayosisi ya Konde, hali inayoashiria hali si shwari ndani ya kanisa hilo.

Marehemu ni baba mzazi wa Askofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ambaye alifariki dunia Jijini Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoani Mbeya kwa mazishi yaliyohudhuriwa na baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo.

Hata hivyo, Askofu Malasusa alipotafutwa kwa simu jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema, “Niko kwenye msiba kwa sasa, ahsante.”

Utaratibu unaofahamika na uliozoeleka ndani ya KKKT ni kwamba mchungaji anayehudumu katika dayosisi anapofariki na kwenda kuzikwa eneo la dayosisi nyingine, dayosisi ya kule anakozikwa ndiye hushughulika na ibada na mazishi.

Hata hivyo, inadaiwa hali ilikuwa tofauti juzi katika mazishi ya mchungaji Malasusa, kwani uongozi wa Dayosisi ya Konde haukushirikishwa na hata Askofu na wachungaji wake 85 walipokwenda kwenye ibada hiyo waliondolewa.

Advertisement “Jana (juzi) limetokea tukio ambalo kwangu kama mkristo limenishtua sana. Askofu wetu (Dk Mwaikali) na wachungaji wake walikuja kwenye ibada ya mazishi, lakini hawakukaa nikaona wanaondoka,”alieleza muumini mmoja aliyekuwepo.

“Nilimuona amekuja ofisa mmoja wa polisi nafikiri ni OCD (mkuu wa polisi wa wilaya) akaongea jambo na Askofu. Nikaona Askofu ametoka nje wakaenda kuzungumza, kidogo wachungaji wote wakaondoka,” alidokeza muumini huyo.

Kwa mujibu wa mchungaji ambaye naye alizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, alidai baada ya Askofu Mwaikali kuondoka, taarifa zilizagaa kuwa yeye na wachungaji wake wametakiwa kuondoka kwa kuwa hawatakiwi.

Mgogoro katika Dayosisi ya Konde unalitikisa kanisa hilo na tayari umezaa kesi ya madai kati ya muumini wake, Afred Kanyiki dhidi ya Baraza la Wadhamini la KKKT, mkuu wa kanisa hilo kubwa nchini, Dk Fredrick Shoo na maaskofu wengine.

Katika kesi hiyo namba 12 ya 2021 iliyofunguliwa Mahakama Kuu Mbeya, Dk Shoo ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, ameunganishwa pamoja na maaskofu wengine sita akiwamo wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Malasusa.

Ni kutokana na mgogoro huo, baadhi ya waumini wanadai pengine ndio kiini cha Askofu Mwaikali na wachungaji wake kutakiwa kuondoka katika ibada, achilia mbali kutoendesha ibada ya mazishi kama utamaduni wa kanisa unavyoelezwa.

Baada ya kuondoka, ibada ya mazishi na shughuli ya maziko iliendeshwa na Askofu Amon Kinyunyu wa Dayosisi ya Dodoma aliyemwakilisha mkuu wa kanisa na gazeti hili lilipojaribu kumtafuta, simu yake ilikuwa imezimwa.

Askofu Mwikali aeleza kilichotokea

Askofu wa Dayosisi ya Konde, Dk Mwaikali alipotafutwa na gazeti hili jana alisita kulizungumzia suala hilo akihoji nani amelipeleka kwa wanahabari, lakini baada ya kuambiwa limeshasambaa katika mitandao ya kijamii, aliamua kufunguka.

“Hata mimi sikujua sana ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, lakini ni kama Mashariki na Pwani (Dayosisi) walijipanga kuendesha ibada yote bila sisi wenyeji kuhusika, kitu ambacho ni makosa.

“Sisi Dayosisi ya Konde hatukuhusishwa na jambo lolote lile. Kawaida msiba kama huu walitakiwa kututaarifu wakiwa kule kule kuwa wanakuja na msiba wa mchungaji, lakini hatukuambiwa,”alieleza Askofu huyo.

Askofu Dk Mwaikali akaongeza kusema “Hata ratiba hatukuiona lakini at the end of the day (mwisho wa siku) nikaambiwa mimi Askofu niondoke kwenye msiba ule na wachungaji wangu wapatao 85 hivi, basi tukaondoka,” alisema.

Kesi ya Askofu Shoo na wenzake

Katika kesi ya msingi namba 12 ya 2021, kupitia kwa wakili Amani Mwakolo, Alfred Kanyiki ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Konde, anawalalamikia Baraza la Wadhamini, Askofu Shoo na wadaiwa wengine tisa.

Wadaiwa wengine ni maaskofu Malasusa, Amos Kinyunyu wa Dayosisi ya Dodoma, Wilson Sanga wa Dayosisi ya Kusini Kati, Blaston Gavile Dayosisi ya Iringa, Renard Mtenji ya Ulanga na Rogath Mollel wa makao makuu ya KKKT.

Kulingana na hati hiyo ya madai, wadaiwa wengine ni Azael Mweleni ambaye ni mwanasheria wa makao makuu ya KKKT, Anicet Maganya ambaye ni mchungaji makao makuu na Askofu Mwaikali ambaye amunganishwa katika kesi.

Katika kesi hiyo, Kanyiki anadai kuwa vikao halali vya Halmashauri Kuu na mkutano mkuu wa dayosisi hiyo, vilifanya uamuzi wa kuhamisha makao makuu wa Dayosisi kutoka Tukuyu kwenda Usharika wa Ruanda Jijini Mbeya.

Uamuzi huu ulipingwa na baadhi ya washarika wa Tukuyu na ndio kiini cha mgogoro ambapo waumini hao wanataka makao makuu yarudi Tukuyu.

Kanyiki anaeleza uamuzi huo haukukiuka kwa namna yoyote katiba ya KKKT na kwamba mkutano mkuu wa Dayosisi ya Konde ndio chombo cha juu cha masuala yote yanayohusiana na uendeshaji wa Dayosisi ya Konde iliyopo Mbeya.

Hata hivyo, analalamika kuwa Agosti 24, 2021 kwa utashi wake mwenyewe, mdaiwa wa pili (Askofu Shoo) aliwateua maaskofu sita (ukimuondoa Mwaikali) na mwanasheria Mweleni na mchungaji Maganya kuunda kamati ya uchunguzi.

Kamati hiyo ilipewa jukumu la kuchunguza mgogoro huo na kuusuluhisha kwa amani na katika taarifa yao, ilikuja na maagizo kuwa makao makuu ya Dayosisi ya Konde yarejeshwe Tukuyu ndani ya siku saba, maagizo yaliyopingwa na dayosisi.

Mdai katika shauri hilo analalamika kuwa Novemba 16,2021, Askofu Shoo na maaskofu wenzake na wajumbe walifika katika dayosisi hiyo na bila uhalali wowote, Askofu Shoo alitangaza kuivunja Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Konde.

Analalamika kuwa siku hiyo Askofu Shoo aliwateua wajumbe hao kushikilia majukumu ya halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Konde na zaidi akabatilisha uamuzi wa mkutano mkuu ulioridhia kuhamisha makao makuu ya dayosisi.

Anadai kuwa hatua ya Askofu Shoo kuivunja Halmashauri Kuu ya dayosisi hiyo ilikuwa ni ukiukwaji wa Katiba ya KKKT Dayosisi ya Konde ya mwaka 2006 na inakiuka Katiba ya KKKT kanuni ya VII G.3 ya mwaka 2015.

Anaeleza katika hati hiyo ya madai kuwa halmashauri hiyo kuu iliyoteuliwa na Askofu Shoo, haitawajibika kwa mkutano mkuu wa Dayosisi ya Konde na itamsababishia hasara ambayo haiwezi kufidiwa kwa thamani ya fedha.

Hivyo anaiomba mahakama mambo 10 ambayo ni pamoja na itamke kuwa Askofu Shoo hana mamlaka ya kuunda kamati ya chaguo lake na pia hana mamlaka kwa mujibu wa Katiba ya KKKT, kuiundia Dayosisi ya Konde kamati ya uchunguzi.

Pia anaiomba mahakama itoe zuio la kudumu kwa wadaiwa wakiongozwa na mkuu wa kanisa, kuacha kuingilia uamuzi wa halmashauri kuu na mkutano mkuu wa Dayosisi ya Konde na pia iwaamuru wadaiwa kulipa gharama za kesi.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz