Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Gwajima apewa onyo kwa uchochezi

97978 Gwajima+pic Askofu Gwajima apewa onyo kwa uchochezi

Thu, 5 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imempa onyo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima baada ya kujiridhisha na kosa la kusambaza kipeperushi na sauti kwa lugha ya kisukuma zenye lengo la kuhamasisha watu kuunda kikundi cha kikabila nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma jana, kipeperushi hicho chenye picha ya Rais Rais John Magufuli kimesambaa kwenye mitandao ya kijamii kikiwa na maandishi yanayosomeka kwa lugha ya kisukuma.

Kaimu kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Camillius Wambura alisema kabla ya onyo hilo walimhoji Askofu Gwajima na baadaye kumuonya kuacha mara moja vitendo vya kuligawa taifa kwa kutumia vigezo vya ukabila.

“Tunatoa onyo kwa wote wenye nia ya kutaka kuligawa taifa kwa njia ya ukabila, udini au ukanda. Tunatoa wito wa kuendeleza umoja na mshikamano uliopo nchini bila kujali dini, kabila wala rangi ya mtu,” amesema Wambura.

Pamoja na kipeperushi hicho, Askofu Gwajima pia alitoa ujumbe wa sauti wenye ujumbe wa kumpongeza Rais Magufuli na kuhamasisha wasukuma kurejesha utamaduni wao wa zamani wa kutumia lugha yao, kusaidiana katika shida na raha.

“Pia, amewataka wasukuma kuunda vikundi kwenye mitandao ya kijamii vya watu elfu mbili (2,000) kwa lengo la kufuatilia watu wanaomtukana mheshimiwa Rais na kuwashughulikia,” alisema Wambura.

Pia Soma

Advertisement
Katika ujumbe huo wa sauti, Askofu Gwajima pia anawataka wasukuma matajiri kuungana pamoja kwa lengo la kuwasaidia wasukuma maskini ili kuondoa dhana ya wasukuma ni maskini na washamba.

Matukio ya Gwajima

Gwajima amekuwa na mikasa ya mara kwa mara na Polisi akihojiwa na kuachiwa kwa tuhuma mbalimbali.

Februari 2017, alihojiwa na Polisi baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akimtaja katika orodha ya wanaojihusisha na dawa za kulevya kabla ya kudai jeshi hilo limethibitika si la kweli.

Kabla ya tukio hilo, mwaka 2015 askofu huyo alianguka na kupoteza fahamu akihojiwa na Polisi kwa madai ya kumtukana na kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Chanzo: mwananchi.co.tz