Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Gamanywa: Tujitenge na mgombea anayesaliti nchi

9742b8129f9cbcd568e12d68f7a1d396 Askofu Gamanywa: Tujitenge na mgombea anayesaliti nchi

Tue, 13 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Jana tulianza kuanza mahojiano haya yaliyofanywa na mwandishi maalumu na Askofu Sylvester Gamanywa baada ya kuzindua kitabu chake kiitwacho Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka Oktoba 7 mwaka huu. Tunaendelea na sehemu ya pili ya mahojiano hayo ambayo Askofu anaelezea kwa kifupi kuhusu maudhui ya kitabu chake. Tuliishia ambapo askofu alisema ziko aina za usaliti, kuanzia usaliti baina ya marafiki, familia na jamii kisha akasema usaliti anaoulenga kwenye kitabu changu ni usaliti dhidi ya nchi. Je, huo ni upi? Endelea naye.

Usaliti dhidi ya nchi

Usaliti dhidi ya Nchi ni kitendo cha mtu au raia wa nchi kutoa ama kwa siri au hadharani, taarifa kwa nia ya kuichongea nchi ionekane vibaya kwa watu wa nchi nyingine au katika anga za kimataifa.

Taarifa hizi za siri mara nyingi hutolewa kwa nia ya kudhalilisha mamlaka ya nchi husika ili mamlaka hayo yatafsiriwe vibaya na nchi nyingine au na jamii za kimataifa. Taarifa za usaliti wa nchi hutolewa kupitia majukwaa yanayotambulika kama ya watetezi wa haki za binadamu, lakini yakiwa yanatumika kama ngazi za vibaraka wa mataifa yenye nia za kuhujumu maslahi ya nchi inayosalitiwa.

Katika miaka ya hivi karibuni mpaka hivi sasa tumeshuhudia baadhi ya watanzania wenye amana ya uongozi wa nchi kwa kupitia vyombo vya habari vya kimataifa wakisema taarifa hasi kwa nia ya kuichonganisha Tanzania ionekane vibaya kwa watu wa mataifa mengine hususan anga za kimataifa. Huu ndio usaliti mkubwa dhidi ya nchi.

Ni Tanzania peke yake duniani nchi ambayo imejaaliwa hekima ya kuchukuliana na wasaliti wa aina hii kiasi hata cha kuwapa fursa ya kugombea tena nafasi za uongozi wa nchi.

Maelezo ya kina kuhusu uzalendo na usaliti nimevichambua ndani ya kitabu nilichokizindua cha Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka. Kila atakayekisoma atajua ukweli wa mambo ulivyo.

SWALI: Askofu unataka jamii iamini kwamba kambi ya upinzani ndiyo wasaliti na chama tawala ndio wazalendo?

JIBU: Suala la usaliti ni mtambuka. Liko vyama vyote kuanzia chama tawala na upinzani, na hata kwa wasiokuwa na vyama kabisa.

Na ikiwa mtu amesoma kitabu nilichokizindua cha Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka bila kujali yuko chama gani au hana chama kabisa, nina hakika hawezi kuacha kumpigia kura ya kumwongezea Rais Dk John Magufuli aendelee kuongoza nchi ili aimalize kazi aliyoianzisha.

SWALI: Huoni maneno haya ya usaliti na uzalendo yanawashambulia watu moja kwa moja?

JIBU: Uzalendo na usaliti sio maneno ya kushambulia bali ni maneno ya “utambulisho wa uhalisia wa mazingira ya kisasa yalipo katika Tanzania” hususan kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Hii ni elimu ya uraia inayohimiza uzalendo na kutahadharisha usaliti na madhara yake.

Watanzania wengi wamezoea kuambiwa uongo na kuushabikia. Ukiwaambia ukweli wanakuchukia kwa sababu ukweli unauma. Ndiyo. “ukweli unauma” na “uongo unaburudisha!”

Lakini jamii inayotaka kurithisha kizazi chake urithi wenye thamani lazima kipaumbele kukizoesha kizazi hicho kuambiwa ukweli unaouma maana hiyo ndiyo itakayokiokoa na majanga yatokanayo na kuaminishwa uongo.

SWALI: Askofu, mpiga kura atajuaje kwamba kura anayokwenda kupiga ni ya uzalendo na si kura ya usaliti?

JIBU: Swali zuri sana. Mpiga kura ambaye moyoni mwake anamfahamu kwa uhakika mgombea wa urais ambaye ana sifa na uzoefu wa kusimamia na kulinda maslahi ya nchi, na kwa sifa hizo akajipanga kwenda kumpigia kura kiongozi huyo, ajitambue kwamba anakwenda kupiga kura ya uzalendo.

Na mpigakura yeyote ambaye anamfahamu mgombea mwenye sifa na uzoefu wa kulinda maslahi ya taifa, lakini kwa sababu za chuki binafsi dhidi ya mgombea huyo, na akampigia kura mgombea mwingine ambaye hana sifa wala uzoefu wa kulinda maslahi ya Taifa, basi ajitambue kwamba anakwenda kupiga kura ya usaliti dhidi ya nchi yake.

Maelezo ya kina kuhusu uzalendo na Maslahi ya taifa nimevichambua ndani ya kitabu changu nilichokizindua.

SWALI: Askofu una uhakika gani kwamba Dk John Magufuli atashinda kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu? Na kwa ushahidi gani wa kitafiti?

JIBU: Katika kuibu swali lako nianze na utafiti kuhusu mwenendo wa kampeni za uchaguzi.

Uhakika wa ushindi wa Dk Magufuli hautokani na ushabiki binafsi wa kisiasa. Nina uhakika kutokana tafiti za kimataifa zilizofanyika kuhusu mwenendo wa kampeni za uchaguzi unaoendelea nchi Tanzania.

Kwa mujibu wa shirika la utafiti la Trends Dynamicues Consulting (ina ushirikiano na taasisi kubwa za kimataifa zikiwemo UNDP, USAID, OXFORD) limefanya tathmini ya mwenendo wa kampeni za uchaguzi unaoendelea nchini Tanzania na kuwasilisha ripoti kama ifuatavyo:

Mgombea wa nafasi ya urais Dk John Magufuli amepata wanaomkubali kuwa asilimia 79 kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na asilimia 80 kwa Tanzania bara tu. Anayemfuatia ni Tundu Lissu ambaye alipata asilimia 19. Hapa kuna kuachana kwa kiasi cha asilimia 60.

Sababu kubwa zilizotolewa za walio wengi kumchagua Rais Magufuli zilikuwa ni uwezo wa kulinda maslahi ya Taifa na uadilifu.

Uadilifu huu ulikwisha kuthibitishwa na ripoti ya Afrika Global Opinion Survey wa mwaka 2019. Katika utafiti huo watanzania walihojiwa kuhusu utendaji wa Serikali ya Dk Magufuli kama kweli inapambana na ufisadi.

Majibu yalionesha kwamba asilimia 72 walijibu kuwa Serikali ya Tanzania kweli inapambana na ufisadi kwa mlinganisho wa asilimia 13 ya mwaka 2015.

Pili, ni ushahidi wa ukuaji wa uchumi. Ripoti ya World Economic Forum, Executive Opinion Survey ya Mwaka 2019, Tanzania imetajwa kuwa ya 28 kati ya nchi 186 duniani zilizofanyiwa tathimini na kudhihirisha umadhubuti katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.

Baadhi ya nchi zilizoachwa mbali na nafasi zao kwenye mabano ni Kenya (70), Uganda (100), Malawi (106), Msumbiji (118), Ghana (61) na Botswana (37).

Rekodi hii inathibitisha kuwa hata dunia inatambua kuwa Rais Magufuli anajenga serikali yenye nidhamu ya matumizi hata kuwa na rekodi kubwa, sio tu Barani Afrika bali duniani kote.

Tathmini ya Benki ya Dunia kwa Tanzania na kuitangaza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imefuzu kuingia kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati duniani, miaka mitano kabla ya mwaka wa kufikiwa lengo hilo ambao ulikuwa 2025 nacho ni kigezo kingine.

Nchi 10 bora zilizo tajiri katika Afrika zilizotajwa miongoni mwa jumla ya nchi 54 za Bara la Afrika ni kama ifiatavyo:

Nigeria inaongoza ikiwa na GDP Dola za Marekani bilioni 446.543, Afrika Kusini inafuata ikiwa na GDP, Dola bilioni 358.839, Misri GDP ya Dola bilioni 302.256 na Algeria yenye GDP inayofikia Dola bilioni 172.781.

Nchi nyingine na kiwango cha GDP kwa dola za Marekani kwenye mabano ni Morocco (bilioni 119,04), Kenya (bilioni 99,246) Angola (bilioni 91,527), Ethiopia (bilioni 91,166), Ghana (bilioni 67,077) na Tanzania ( bilioni 62,224).

Vyanzo vya takwimu ni Shirika la Fedha diniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB).

Tatu, ni utunzaji wa amani na utulivu wa Tanzania chini ya Rais Magufuli.

Tukienda kiutafiti tunapata ripoti ya mwaka 2020 ya Global Peace Index ambayo imetangaza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 bora za kiafrika zenye amani duniani.

Katika 10 bora Tanzania imeshika nafasi ya 7 na imeshika nafasi ya 1 katika Afrika Mashariki. Orodha ya nchi 10 bora za kiafrika zinazoongozwa kwa amani na utulivu kwa kuanza na ya kwanza hadi ya kumi ni Mauritius, Botswana, Ghana, Zambia na Sierra Leone.

Nyingine ni Senegal, Tanzania (ambayo ni ya kwanza katika Afrika Mashariki), Namibia, Liberia na Malawi. Chanzo ni www.africanvibes.com

Pamoja na ushahidi huu wa kitafiti, lazima niitahadharishe jamii kuhusu viashiria vinavyotishia kuvunjika kwa amani na utulivu, tena kwa kupitia mwavuli wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz