Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Chengula akumbukwa kwa misimamo yake, kuzikwa Jumanne

28419 Askofu+pic TanzaniaWeb

Fri, 23 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Viongozi na wananchi wa jiji la Mbeya wamesema kifo cha Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Mhashamu Evarist Chengula (pichani) kimeacha simanzi na wamempoteza kiongozi muhimu wa kiroho.

Askofu Chengula alifariki dunia juzi asubuhi wakati akipatiwa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es salaam.

Askofu Chengula atakumbwa kwa mengi, hasa ujumbe aliokuwa akiutoa kwa wananchi na waumini kuhusu masuala mbalimbali, hasa uwajibikaji katika nchi yao.

Akihubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu Machi 30, Askofu Chengula aliwataka Wakristo kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa mwakani kwa kuchagua watu ambao hawatawafanya waishi kwa kuogopaogopa.

Katika ibada hiyo iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Fatma, Mwanjelwa jijini Mbeya na kuonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa (TBC1), Askofu Chengula alisema ujumbe uliokuwa umetolewa na maaskofu siku kadhaa zilizopita ulikuwa haumlengi mtu fulani, bali wanafiki wanaodai ni Wakristo, lakini hawana imani ya dini hiyo ili waweze kubadilika na kuwa watu wema.

“Tuangalie, kulialia tu hakuna maana. Tufikiri kabla ya utendaji kitu, sisi maaskofu tumeona udhaifu wetu ni huu, kila mara baada ya uchaguzi ndiyo tunaanza kum – analyse (kumchambua) mtu, kumtathmini mtu kwamba ataweza au hawezi.

“Hakuna maana tufurahie watu fulani tumewachagua, lakini tunaishi katika hali ya wogawoga, sasa wote tunaanza uchaguzi wa mwaka kesho,” alisema.

Jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima alisema Askofu Chengula atazikwa Mbeya Jumanne ijayo.

Alisema ibada ya mazishi itafanyika Jumatatu jijini Dar es Salaam kabla ya mwili wa marehemu kusafirishwa kwenda Mbeya.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, viongozi na wananchi wa jiji la Mbeya walisema Askofu Chengula alikuwa mtu muhimu kutokana na uimara wa kusemea, kukemea na kusimamia kile alichokiamini katika utumishi wake wa kiroho.

Mbunge wa Songwe, Philip Mulugo alisema Askofu Chengula alikuwa kiongozi asiyefungamana na mrengo wowote wa kisiasa lakini alikuwa mshauri mkubwa wa wanasiasa.

“Nilimfahamu vizuri sana baba Askofu tangu siku ya kwanza akisimikwa kuwa askofu wa Jimbo la Mbeya mwaka 1997 pale Kanisa la Mwanjelwa. Katika uongozi wake alikuwa mkweli alikuwa hafungamani kabisa na masuala ya kisiasa,” alisema Mulugo.

Kauli ya mbunge huyo wa CCM aliungwa mkono na Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akisema, “Baba Askofu Chengula hakuwa kiongozi tu wa kiroho yule alikuwa ni baba wa Mbeya hii, alikuwa ni mshauri mkubwa sana kwa viongozi wakubwa tu Mbeya hii.”

“Hili ni pigo kubwa sana kwetu Mbeya, nuru yetu imezima ghafla mno. Mara ya mwisho Baba Askofu alikuja nyumbani kwa mama yangu kunisalimia baada ya kufariki, aliniambia vitu vingi mno na mwisho akaniahidi kuja nyumbani kwangu Ituha kunywa wine, najua alikuwa na jambo zito alilotaka kunieleza tukiwa nyumbani kwangu,” aliongeza Sugu.

Mbunge huyo alisema baada ya Bunge kuzuiwa kuonyeshwa moja kwa moja ‘live’ Askofu Chengula alimuita ofisini kwake na katika mazungumzo hayo alionekana kutopendezwa na uamuzi huo.

Imamu Msaidizi wa Msikiti Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Katanga alimwelezea Askofu Chengula kwamba, “Alikuwa mshauri mkubwa na alikuwa kiongozi wa kiroho aliyesimama katika ukweli siku zote, alituunganisha wananchi wa Mbeya bila kujali tofauti zetu za kidini.”

Muumini wa Kanisa Katoliki ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Tawi la Mbeya, John Stevin alisema vijana wengi watamkumbuka Askofu Chengula kutokana na ucheshi na kuwa karibu nao siku zote.



Chanzo: mwananchi.co.tz