Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu Bagonza atoa ujumbe mzito

89137 Bagonza+puic Askofu Bagonza atoa ujumbe mzito

Thu, 19 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza amesena mwanadamu hawezi kumpenda Mungu kisha akamdharau na kumtesa mwanadamu mwenzake.

Katika salamu zake za sikukuu ya krismas kwa mwaka 2019 na za mwaka mpya wa 2020 alizozisambaza kwa waumini jana, Askofu Bagonza anasema Mungu na mwanadamu wameshikamana.

Salamu hizo ambazo ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka wa maaskofu wa KKKT, Katoliki na Makanisa mengine zimetumwa kwa waumini wote wa Dayosisi ya Karagwe.

“Kumpenda Mungu huku tukiwatesa na kuwadharau wanadamu ni ibada ya sanamu na Mungu hawezi kuwa upande wetu hata kama tunamuimba kila siku na kula viapo kwa jina lake,” alisema Askofu Bagonza na kuongeza:

“Tunaalikwa kuheshimu utu wa mwanadamu kama Mungu alivyouheshimu na kufanyika mwili. Kumtesa mwanadamu ni kumtesa Mungu aliyefanyika mwili.

“Kumdhulumu, kumbeza, kumbagua, kumnyanyasa mwanadamu ni sawa na kumtendea Mungu mambo hayo kwa sababu Mungu yupo ndani ya mwanadamu.

“Tunaalikwa kuwa watetezi wa haki kwa sababu ndani ya mtu, yumo Yesu aliyezaliwa kwa ajili ya ulimwengu wote. Tuache hila na uongo na tuukumbatie ukweli uletao uhuru kamili.”

Askofu Bagonza alisema kuzaliwa kwa Yesu Kristu kulileta mtizamo mpya katika hali ya dunia na thamani ya binadamu iliongezeka kwa kubeba sura ya Mungu na ukweli ulipata mmiliki halisi.

“Uzima wetu umo mikononi mwa Yesu Kristo aliyezaliwa. Uhai wetu waweza kutoweka lakini uzima utabaki daima kwa sababu ni mali ya Mungu. Noel ni Immanuel yaani Mungu pamoja nasi.

“Mungu si Mungu bila watu na watu si watu bila Mungu. Ndani ya Mungu kuna watu na ndani ya watu kuna Mungu. Kwa hiari yake Mungu alifanyika mwili ili tuunge Umungu sisi wanadamu,” alisema.

“Shughuli za kisiasa kama vile maandamano, mikutano ya hadhara, ambayo ni haki ya kila raia, vinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola”,unasomeka sehemu ya waraka huo wa Maaskofu.

Waraka huo ulitaja mambo mbalimbali uliodai ni tishio la amani na umoja wan chi kuwa ilikuwa ni kuibuka kwa vitendo vya utekaji, utesaji, kupotea kwa watu na matumizi mabaya ya vyombo vya dola.

Maaskofu hao waligusia kile walichodai ni kutoweka kwa Uhuru wa kujieleza na wakaonya juu ya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi.

Katika uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi ya Kati mjini Tabora, Makamu wa Rais, Samia Suluhu alisema Serikali haina ugomvi na dhehebu lolote na ipo tayari kukosolewa kwa kutumia lugha ya staha.

Chanzo: mwananchi.co.tz