Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anthony ashindwa kwenda likizo Ngara

33699 Anthony+pic Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ngara. Ndoto za mtoto Anthony Petro kwenda likizo wilayani Ngara kuonana na baba na dada zake zimegonga mwamba, baada ya kukosekana fedha za kumsafirisha.

Anthony kwa sasa yuko wilayani Mwanga, Kilimanjaro anakosoma katika Shule ya Amani Vumwe English Medium baada ya kujitokeza msamaria mwema anayemfadhili kimasomo.

Akizungumzia hatua hiyo, mfadhili huyo Isihaka Msuya, alisema kwa sasa Anthony amempeleka nyumbani kwake hadi shule itakapofunguliwa ambapo atamrudisha shuleni.

Msuya alisema katika mkataba wa ufadhili wa masomo kwa mtoto huyo, Halmashauri ya Ngara ilitakiwa kubeba jukumu la kumrudisha nyumbani wakati wa likizo na kumpeleka shuleni inapomalizika.

“Hapa nyumbani kwangu atapata huduma zote sawa na watoto wangu kinachotakiwa ni kumuendeleza apate elimu ya kuweza kumkomboa na kumfanya afikie ndoto ya kuwa na maisha bora,” anasema Msuya.

Halmashauri yafafanua

Ofisa ustawi wa jamii wilayani Ngara, Mussa Balagondoza na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Aidan Bahama kwa nyakati tofauti walisema changamoto inayowakabili ni kutopatikana kwa fedha.

Hata hivyo, Balagondoza alisema ilikuwa muhimu wakati Anthony anakabidhiwa kwa mkurugenzi wa hamashauri ya wilaya ya Mwanga kuweka utaratibu wa kumsafirisha hadi nyumbani wakati wa likizo ili Ngara iwe na jukumu la kumpeleka shuleni likizo inapomalizika.

“Kwa siku kadhaa nilikuwa Bukoba siwezi kueleza zaidi kuhusu jambo hili, tuvumilie mwaka huu umekwisha lakini mwakani naamini zitafanyika taratibu ili Anthony arudi nyumbani kwao kusalimia wazazi na ndugu zake,” alisema Balagondoza.

Viongozi wa halmashauri hiyo wakati Anthony anaanza kutambulika kwenye mitandao ya kijamii kwa ujasiri wa kutishia kumshtaki baba yake endapo angeuza shamba, waliahidi kumnunulia shamba lingine, kumjengea nyumba na kumsomesha.

Baba apangiwa nyumba

Katika hatua nyingine wasamaria wema wamejitolea kumpangia nyumba Mzee Petro Magogwa ambaye ni baba wa Anthony anayeishi Kijiji cha Ngundusi wilayani Ngara baada ya nyumba iliyoanza kujengwa na wafadhili kutokamilika ikiwa sasa inakaribia miezi saba.

Katibu wa Kikundi cha Tumsaidie Anthony Petro, Stella Rutaguza alisema tayari nyumba imepatikana ambapo mzee huyo ataishi kwa muda na familia yake.

“Nyumba iliyopatikana inalipiwa Sh25,000 kwa mwezi mmoja na imelipiwa miezi minne. Tunaamini itamwezesha kuishi na watoto wake wawili wa kike katika mazingira yenye usalama kwa kuwa ipo katikati ya kijiji. Aidha, itawawezesha watoto kwenda na kurudi shuleni kwa urahisi wakipita kwenye njia zisizo hatarishi,” alisema.

Pia, alisema kikundi hicho kimemnunulia mzee huyo shamba la migomba kwa gharama ya Sh2 milioni.

Nao mfuko wa Tumaini ulio chini ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera makao makuu Murgwanza, umewanunulia sare na vifaa vya shule dada zake Anthony, Editha na Eliza wanaotarajiwa kuingia darasa la tatu mwakani 2019 katika Shule ya Msingi Ngundusi.

Mratibu wa mfuko huo Alex Nyamkara, alisema walianza muda mrefu mchakato wa kutaka kuisaidia familia ya Mzee Magogwa, lakini kutokana na mkanganyiko wa hapa na pale katika uratibu wa misaada kwa familia hiyo walilazimika kusubiri hali ikae sawa.

“Awali tulidhamiria kuandaa andiko kwenda kwa wafadhili wa mfuko huu nchini Uingereza ili wasaidie kupatikana fedha za kununua shamba na kumjengea nyumba, lakini baadae tulipata taarifa kuwa amepatikana mfadhili atakayeijengea familia hiyo nyumba.

“Kadri tutakavyopata fedha za kusadia watu wanaoishi katika mazingira magumu tutatenga fungu ili kuwasaidia dada zake Athony. Hatutashindwa kuwanunulia sare za shule na vifaa vya masomo ili wawe sawa na wenzao darasani,” alisema Nyamkara.

Anthony alipata umaarufu kupitia mitandao ya kijamii baada ya picha na video yake kusambaa mitandaoni akimtishia baba yake kumpeleka kituo cha polisi Kabanga baada ya kumuona akiwa katika harakati za kuuza shamba alilosema ndio rasilimali pekee wanayoitegemea katika familia yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz