Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyejifanya mganga, mhubiri mikononi mwa polisi

27075 Pic+mhanga TanzaniaWeb

Wed, 14 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Idara ya Uhamiaji mkoani Mara imekamata wahamiaji haramu wanane akiwemo mwanamke mmoja kutoka nchini Kenya aliyekuwa akiishi na kufanya shughuli za uganga wa kienyeji na kuhubiri injili kwa wakati mmoja.

Mwanamke huyo raia wa Kenya alikamatwa wilayani Bunda akijihusisha na masuala ya uganga wa kienyeji huku akijifanya kuwa ni muhubiri wa neno la Mungu.

Ofisa Uhamiaji mkoa wa Mara Frederick Kiondo amesema mjini hapa leo Novemba 14 kuwa mbali na mwanamke huyo idara yake pia imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu wengine saba raia wa Ethiopia.

Amemtaja mwanamke huyo kuwa ni Wego Carolina Anyango (54) ambaye anadaiwa kufanya shughuli za uganga wilayani Bunda huku wateja wake wakubwa wakiwa ni watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kama vile wizi.

Amewataja wahamiaji wengine waliokamatwa kuwa ni pamoja  na Shifaru Belu (25), Damec Abain  (23), Danlyi Kifile  (23), Dageka Abara  (27), Yisk Shobeso(20), Teshade Abirham  (22) na Bekele Sayoko (43) wote raia wa Ethiopia.

Kiondo amesema kuwa wahamiaji hao  kutoka Ethiopia wamekamatwa mwanzoni mwa wiki hii wakiwa wamefichwa kwenye vichaka katika kijiji cha Kirumi wilayani Butiama ili baadaye wakachukuliwe na gari na kusafirishwa kwenda jijini Mwanza na  kisha kuelekea nchi za Kusini mwa Afrika .

Amesema kuwa wakati raia hao wa Ethiopia wakikamatwa, mwanamke huyo alikamatwa wilayani Bunda na kwamba hii ni mara ya pili kwa Idara ya Uhamiaji kumkamata mama huyo na kisha kumrudisha nchini kwao.

Kiondo amesema kuwa wahamiaji wote watarejeshwa makwao na endapo watarudi tena nchini bila kufuata taratibu watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.



Chanzo: mwananchi.co.tz