Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Africraft; Wajasiriamali wanaotajirika kupitia taka rejereshi

61890 TAKA+PIC

Mon, 10 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bagamoyo. Unafahamu kuwa nchini Tanzania kwa mwaka zaidi ya chupa milioni 300 hutupwa? Lakini bahati mbaya ni kwamba taka hizo zitachukua miaka zaidi ya 500 kuoza.

Hii ni tofauti na mifuko ya plastiki ambayo haiwezi kabisa kuoza, ambayo Juni Mosi, 2019 Serikali ilipiga marufuku mifuko hii kutumika.

Mwishoni mwa wiki MCL Digital ilikutana na vijana wanaotengeneza bidhaa zao za pekee kama vioo vya urembo, glasi za maji kutokana na chupa za soda na mvinyo, vyakuegeshea mishumaa kutokana na vifuu vya nazi, mabegi ya kubebea kompyuta mpakato na vifaa vingine na kadhalika.

Bidhaa hizo zinazotengenezwa na kikundi cha AfriCraft kupitia rasilimali rejereshi ambazo  zimerejereshwa kutoka kwenye takataka kama plastiki.

Gillan Oppy ni mmoja kati ya vijana wa Kitanzania kutoka AfriCraft ambao wameamua kujikita katika utengenezaji wa bidhaa hizo kwa kutumia mifuko ya sarufi, chupa za bia na mvinyo, vifuu vya nazi na takataka zinginezo.

“Tupo zaidi ya 20, mimi na wenzangu tulitafakari namna gani tunaweza kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, tukaona ni vema tutumie ufahamu tulionao kubuni bidhaa kupitia malighafi ambazo wengi huzitupa baada ya kumaliza muda wa matumizi,” amesema Oppy.

Pia Soma

Amesema wazo lao ni la tofauti kidogo na wengi wanavyodhani, kwani hutumia makopo yaliyokwishatumika hasa yale ya soda za kopo, vifuu, chupa, mifuko ya plastiki, viroba vya unga wa ngano na sembe na ile ya saruji.

“Utaona malighafi hizi wengi huzitupa baada ya kuzitumia na kutokana na hali hiyo, taka hizo zimekuwa zikichangia mno uharibifu wa mazingira yetu,” amesema.

Oppy amesema soko lao kubwa la bidhaa wanazotengeneza ni Ujerumani na Marekani na hata nchi zingine kadhaa, lakini ndani hakuna soko linalojitosheleza.

Amesema wao wametengeneza vitu vingi kupitia taka hizo na hata kujenga nyumba za kupendeza maeneo mbalimbali kupitia chupa za plastiki ikiwemo Msasani na SlipWay.

Suala hilo linaungwa mkono na Mmiliki wa Firefly Lodge, Bagamoyo Beach Lovers, Joanna Turner ambaye amesema kufuatia uchavuzi wa mazingira, miaka mitatu iliyopita aliamua kuunda kiwanda kidogo cha kukusanya malighafi rejereshi ili kuokoa mazingira katika fukwe za Bagamoyo.

Amesema ametenga eneo maalum ambalo anakusanya taka hizo, “Tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha tunatunza ardhi na bahari, hivyo niliamua kuanza kutoa elimu kwa watu mbalimbali ili kutokomeza uchafu au taka rejereshi kwa kuzikusanya pamoja.

“Nimeanzisha sehemu ndogo ambayo nakusanya taka hizo kulingana na aina na kisha watu kutoka Dar es Salaam huja kuzichukua hapa kwangu na kwenda kuzirejeresha kwa kutengeneza chupa mpya, ndoo, mabeseni na hata viti vya plastiki, lakini vikitupwa hovyo vitaharibu mazingira,” amesema Turner.

Tunner amesema kuna hatari kubwa kwa vizazi vijavyo ikiwa taka hizi hazitatafutiwa namna mpya ya kuzitokomeza au kuzirejeresha upya, akitolea mfano wa chupa ya plastiki ambayo huchukua hata miaka 500 kuoza.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz