Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ALHAMISI KUU Yuda Iskariote na dhana ya usaliti dhidi ya upendo 

Bab433f946950b767407d814a5d6b53a.jpeg ALHAMISI KUU Yuda Iskariote na dhana ya usaliti dhidi ya upendo 

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

LEO ni Alhamisi Kuu, Wakristo duniani wanaanza adhimisho lililo kuu kuliko maadhimisho yote la Kiliturujia (pia unaweza kuita liturugia), adhimisho lililo chanzo cha maadhimisho yote ya kiliturujia.

Liturujia ni neno lenye asili ya Kigiriki au Kiyunani likiwa limejengwa kutokana na maneno mawili: ‘laόs’ maana yake watu na ‘ergon’ maana yake kazi.

Kwa hiyo liturujia maana yake ni kazi ya watu au huduma yoyote aliyoitenda mtu kwa manufaa ya watu au umma. Kazi hiyo iliweza kuwa mtu anaitenda kwa hiari yake au kwa lazima, yaani kwa mujibu wa sheria.

Biblia ilipotafsiriwa katika Kigriki kutoka lugha ya Kiebrania neno liturujia limetumika mara nyingi kumaanisha huduma takatifu iliyotolewa na makuhani wa kabila la Lawi kwa Mwenyezi Mungu.

Hivyo, hili ni adhimisho la fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana Yesu Kristo. Liturujia yote ya Kanisa inachota maana yake katika msingi huo.

Adhimisho hili ni la siku tatu, yaani: Ijumaa Kuu inayoanzia siku ya Alhamisi Kuu jioni kwa tukio la ‘Karamu ya mwisho’, Jumamosi Kuu na Jumapili ya Pasaka.

Katika adhimisho la jioni ya Alhamisi Kuu mambo matatu yanapewa uzito na tafakari ya kina katika kuelekea sherehe ya ufufuko wa Bwana Yesu Kristo (siku ya Pasaka).

Kwanza, huadhimisha Karamu ya Bwana Yesu Kristo, karamu hii huitwa Karamu ya mwisho ikiwa na maana ni Karamu ya mwisho ya Pasaka, ambayo Yesu Kristo alikula pamoja na wanafunzi wake kabla ya kukamatwa kwake, kuteswa na hatimaye kufa msalabani.

Hivyo, katika nafasi ya kwanza Wakristo hutakiwa kufakari ukuu wa karamu hii ya kipasaka, karamu ambayo tofauti na Pasaka ya Wayahudi, Yesu Kristo kama mkuu wa kaya anaweka kitu kipya ambacho kinawapatia mwanzo mpya.

Pili, ukitazama kwa makini utagundua tena uwepo wa maadhimisho mengine mawili ya siku ya Alhamisi Kuu. Yesu Kristo katika kuuweka mwili wake na damu yake alimalizia kwa kusema: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (badala ya kuendelea kuwa ukumbusho wa Musa na jinsi alivyowakomboa Waisraeli kutoka Misri).

Agizo hili la kuendeleza karamu hiyo ya kipasaka linatupeleka mara moja katika kutafakari ni kwa namna gani mlo huo utafanywa kuwa ni wa kudumu katika jamii ya mwanadamu.

Jambo la tatu ambalo Wakristo wanaliadhimisha katika siku hii ya Alhamisi Kuu ni Amri ya Mapendo. Hii ni ishara ya Umoja na kifungo cha Upendo.

Katika somo hili Yesu Kristo anatoa fundisho la namna ambayo upendo huo unapaswa kuwa; ni upendo wa kujitoa katika ukamilifu wote, kujisadaka katika uhuru wako mithili ya mtumwa.

Namna yake ya utumwa ni tofauti na utumwa ulivyozoeleka. Anajitoa katika hali ya utumwa kwa uhuru wote na mapendo makubwa.

Katika karamu hiyo, Yesu alitoa maneno yake ya buriani kwa wanafunzi hao akikazia kuhusu amri mpya ya kwamba wapendane kama jinsi ambavyo yeye alivyowapenda.

Yesu anatambua wazi kwamba yeye ni Bwana na mwalimu wao, ni mkuu wao na kwa desturi hakupaswa kuwaosha miguu walio chini yake.

Kwa kitendo cha kuwaosha miguu wanafunzi wake anatupatia shule kubwa sana ya namna ambavyo tunapaswa kujitoa kuwahudumia wengine katika hali ya upendo mkamilifu.

Yesu Kristo alijitoa kuwahudumia wengine waliokuwa mbele yake na waliohitaji huduma yake bila kuangalia nguvu zake, mamlaka yake, uwezo wake na kadhalika.

Namna hii ya Upendo wa Yesu, inatuondoa katika kuhudumiana kwa ubaguzi wa namna yoyote na inatuleta katika umoja wa wana wa Mungu.

Kitu cha kushangaza ni kwamba pamoja na kujua kwamba yupo mmoja atakayemsaliti kati ya wanafunzi wake, Yesu bado hakuacha kuonesha upendo huo mkuu.

Lakini leo hii, tulio wengi tumeshindwa kuishi maisha ya upendo, hatuwaangalii kabisa wengine walio mbele yetu na wanaohitaji huduma yetu, wakiwa na hakika ya kupatiwa huduma hiyo kutoka kwetu.

Tumekuwa tukiishi maisha ya usaliti, tukisaliti ndoa zetu, tukiwasaliti ndugu zetu na kwa taifa letu. Usaliti ni miongoni mwa mambo mabaya zaidi yaliyoenea leo. Usaliti ni ishara yenye kuogopesha ya siku za mwisho.

Usaliti ni tendo la kutoa siri za mtu, kikundi au nchi kwa adui wa mtu, kikundi au nchi hiyo. Mara nyingi mtendwa wa usaliti hupata maumivu makali, wakati huo huo mwanzoni msaliti hukenua kwa kudhani ameshinda, ingawa maisha hayapo hivyo!

Anayesalitiwa humwaga machozi kwa kilio cha mahangaiko ya moyo. Husahau kumshukuru Mungu. Hutamani kulipa kisasi.

Hushindwa kutambua kuwa mzunguko wa maisha ya binadamu kama Mungu alivyoumba, tendo baya humrudia mtendaji mwenyewe wasaa unapotimu-KARMA!

Laiti kila mmoja angejua mataabiko ambayo wasaliti hukutana nayo baadaye, kungekuwa na nafuu kubwa ya kimaisha na idadi ya vitendo vya usaliti ingepungua.

Msaliti anapaswa kujua; Unapomsaliti mwenzio maana yake unakuwa sawa na kuyageuza maisha yake juu chini. Hilo si jambo dogo, kwani unaharibu mfumo wa maisha yake. Maumivu unayompa ni makubwa mno.

Dhana hii ya usaliti inatukumbusha kisa ndani ya Biblia kinachomhusu Yuda Iskariote. Huyu alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Yesu, aliishi, kula na kunywa na Yesu.

Yuda Iskariote alimjua vyema Yesu, kwani kwa zaidi ya miaka mitatu alikuwa akiambatana naye kama mwanafunzi na rafiki mtiifu wa mwalimu. Mwishowe Yuda alimsaliti Yesu.

Biblia inaeleza kuwa Wayahudi walipopanga kumkamata Yesu na kumsulubisha msalabani, hawakuwa wakimjua vizuri kwa kuwa alifanana sana na wanafunzi wake.

Hivyo, Wayahudi walimshawishi Yuda Iskariote kwa kumpa vipande thelathini vya fedha ili awaoneshe yupi ni Yesu katika kundi la wale Thenashara (Mitume kumi na wawili kama neno la Kigiriki “dodeka”).

Pasipo ajizi Yuda Iskariote alikubali kumsaliti Yesu kwa vipande thelathini vya fedha. Ni wazi kuwa tamaa na ushawishi wa fedha ndiyo uliomvutia Yuda Iskariote kumsaliti Mwalimu wake.

Kama nilivyobainisha mwanzoni mwa makala yangu kuwa, tendo baya humrudia mtendaji mwenyewe wasaa unapotimu, vivyo hivyo, baaada ya usaliti huu, Yuda Iskariote msaliti wa Yesu aliumia sana roho yake.

Aliumia kwa kuwa aligundua kuwa alimsaliti mwenye haki asiye na hatia wala makosa yaliyostahili mateso na kuuawa.

Biblia inasimulia kuwa Yuda baada ya kubaini kuwa alifanya kosa kumsaliti mwenye haki, alikwenda kurudisha zile fedha kwa watesi wa Yesu na kujinyonga hadi kufa.

Naam, usaliti ulimuua Yesu na Yuda Iskariote. Usaliti haukumuacha salama Yuda Iskariote.

Hatuiishi kwenye usaliti tu, bali tumejawa ubinafsi na ufisadi. Ufisadi umeenea na kuwa tata sana, kiasi kwamba unatisha kuharibu misingi ya jamii. Katika nchi fulani haiwezekani kufanyiwa lolote bila kutoa rushwa.

Wengine hutoa rushwa kwa watu wenye mamlaka ili kupita mtihani, kupata leseni ya kuendesha gari, kupata kandarasi, au kushinda kesi. Ufisadi ni kama uchafuzi mkubwa unaovunja mioyo ya watu.

Hivyo, wakati tukiiadhimisha siku hii ya Alhamisi Kuu tunapaswa tujiulize: Je, ni mambo gani yenye kuonya tunayoweza kujifunza kutokana na usaliti wa Yuda Iskariote?

0685 666964 au [email protected]

Chanzo: www.habarileo.co.tz