Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

292 waumwa na mbwa wilaya ya Ulanga, Malinyi 2019

77614 Mbwa+pic

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu wanne wamepoteza maisha na wengine 288 kupata majeraha wilaya ya Ulanga na Malinyi Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania baada ya kuumwa na mbwa kuanzia Januari mpaka Agosti mwaka huu.

Akitoa tamko katika siku ya kichaa cha mbwa duniani leo Jumamosi Septemba 28, 2019, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema mashambulizi hayo yametokana na mlipuko wa kichaa cha mbwa katika wilaya hizo.

“Mwaka huu 2019, kuanzia Januari hadi Agosti, watu 16,290 wametolewa taarifa ya kuumwa na mbwa na vifo nane vimeripotiwa kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa, mlipuko ulitokea Malinyi na Ulanga na watu 292 wameumwa,” amesema Ummy Mwalimu.

Hata hivyo, amesema tatizo la kichaa cha mbwa ni kubwa zaidi ya takwimu hizo, kwani hazijumuishi vifo vinavyotokea nyumbani na waathirika ambao hawakufika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Amesema utafiti uliofanyika mwaka 2002 nchini Tanzania ulibainisha kuwepo takriban vifo 1,499 kwa mwaka kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

“Katika kudhibiti mlipuko huu, kupitia Dawati la Afya Moja, Wizara ya Mifugo ilipata chanjo 16,000 kwa ajili ya kuchanja mbwa.  Zoezi la kuchanja mbwa lilitekelezwa Mwezi Aprili hadi Mei, 2019.”

Pia Soma

Advertisement
Aidha amesema elimu ya kujikinga dhidi ya kichaa cha mbwa ilitolewa kwa shule za msingi na viongozi wa kata.

Amesema tafiti zimeonyesha waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto chini ya miaka 15, kwa sababu wao ndio wanaokuwa karibu zaidi na mbwa (anayefugwa) na pia hupenda kucheza/kuchokoza mbwa wasiowafahamu njiani.

Aprili 2018 ulitokea mlipuko wa ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo watu sita waliumwa na mbwa na kati yao wanne walichelewa kwenda kupata chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa, hivyo waliugua na walipoteza maisha. 

Kuhusu kichaa cha mbwa

Vimelea vya kichaa cha mbwa vinapoingia katika jeraha hushambulia neva za fahamu kutoka katika eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimaye kuathiri ubongo. 

Dalili  za ugonjwa wa kichaa cha mbwa huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa fahamu na baadaye ubongo, ambazo ni pamoja na kuwashwa sehemu ya jeraha, homa, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa na mate mengi mfululizo, kuweweseka (kushtuka mara kwa mara na kuogopa), kupooza na hatimaye kupoteza maisha.

Wakati mwingine watu huhusisha dalili hizi na imani za kishirikina, hivyo hawaendi katika vituo vya kutolea huduma za afya, hutibiwa kienyeji hadi kupoteza maisha wakiwa nyumbani.

Chanzo: mwananchi.co.tz