Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

vifaa vya ujenzi changamoto ya miradi Longido

874ba89bccb10a60b54bb88dc8497457.jpeg vifaa vya ujenzi changamoto ya miradi Longido

Sun, 21 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk Athumani Kihamia amesema Wilaya ya Longido ni moja ya wilaya iliyopewa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule shikizi kutokana na jiografi a ya eneo hilo na kutoa wito kwa wasimamizi wa ujenzi kutofanya ubadhirifu wa fedha hizo.

Dk Kihamia alisema wilaya hiyo imepewa Sh bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 50 maeneo mbalimbali katika wilaya na kuwa fedha hizo ni za moto na wasijaribu kuzitumia kinyume na kile kilichoagizwa.

Akizungumzia hali ya miradi inavyotekelezwa alisema pamoja na kuwa wilaya hiyo upatikanaji wa nyenzo kwa ajili ya ujenzi ni changamoto, lakini viongozi wamejitahidi kusimamia tofauti na maeneo mengine ambayo malighafi zinapatikana kwa haraka.

“Mmejitahidi na mpo kwenye hatua nzuri, lakini haimaanishi kuwa mmeshamaliza kazi bado, tutarudi kukagua na wataendelea kuja watu kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kukagua miradi hii ikiwemo Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa),” alisema. Katika hatua nyingine, aliwaasa wazazi kuwapeleka watoto shule na kuachana na desturi ya kuwachungisha mifugo.

Alisema serikali inatambua haki ya elimu kwa mtoto ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan alitoa fedha za ujenzi wa madarasa hayo kuwasogezea huduma karibu watoto wasiendelee kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

Mkazi wa Kata ya Orbomba, Tarafa ya Longido, Jacob Laizer akizungumza kwa niaba ya wananchi alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuleta fedha za miradi ya elimu.

Alidai kuwa shulenyingi wilayani humo zenye ufaulu duni wa watoto ni kutokana na umbali mrefu kwenda shule. Alisema uwepo wa shule hizo karibu na jamii kutasaidia kupunguza uzorotaji wa elimu kwa watoto wa jamii ya kifugaji, kwani uvivu wa kutembea zaidi ya kilometa 10 hadi 25 kufuata elimu utapungua na watoto watasoma kwa raha.

“Hata hivyo, watoto wetu walipokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu kwenye shule mama za msingi walikuwa wakikutana na wanyama wakali hali hiyo pia ilikuwa ikiwatia hofu na kukata tamaa ya kuendelea na masomo na kusababisha utoro sugu wa wanafunzi,” alisema Laizer.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Nurudin Babu katika ziara yake alisisitiza jamii hiyo kutumia majengo hayo yatakapokamilika kwa kuhakikisha watoto wanakwenda shule. Aidha, aliitaka jamii kujiongeza kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika maeneo yaliyojengwa shule shikizi sambamba na madarasa hayo ili watoto watakapoanza kusoma wapate huduma na kuepuka kujisaidia maeneo yasiyo rasmi mfano vichakani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Longido, Stephen Ulaya alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa maji na matofali, lakini wamejipanga kukabiliana nalo na ifikapo Desemba 15 madarasa hayo yatakuwa yamekamilika. “Ikumbukwe kuwa fedha hizi ni fedha za mpango wa serikali ya Tanzania wa kuinua uchumi kwa kutumia mkopo wa fedha wa Sh trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live