Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zumaridi afutiwa kesi, sasa yupo huru

Z55 Zumaridi huru kesi usafirishaji binadamu

Thu, 9 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na madai hayo, ameomba shauri hilo kuondolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.

Shauri hilo lililokuwa limepangwa kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi ili kwenda Mahakama Kuu kusikilizwa ushahidi wake Februari 9, mwaka huu, lilisikilizwa kwa dharura jana katika chemba ndogo ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Boniventure Lema.

Akisoma uamuzi huo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Dorcus Akyoo, amesema DPP alifikia uamuzi huo kutokana na kifungu cha sheria namba 90 kifungu kidogo namba 11 Sura ya 20 ya Mwenendo wa Mashahidi kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lema amemwachia huru Zumaridi katika kesi hiyo namba 11/2022.

"Sasa uko uhuru katika kesi hii namba 11/2022, hivyo unaweza kuendelea na shughuli zako lakini hii haitoathiri shauri lilokuweka hatiani," alisema Lema.

Baada ya uamuzi huo, Wakili aliiomba mahakama kupokea maombi ya serikali juu ya kuomba awe chini ya uangalizi katika kipindi cha miaka mitatu bila kujihusisha na masuala yoyote ya uvunjifu wa sheria na amani katika maeneo yake sambamba na kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) wa Mwanza  mara moja kila mwezi.

Alisema maombi hayo yalitolewa chini ya kifungu cha sheria namba 70 na 72 kifungu kidogo 'e' pamoja na kifungu namba 74 na 370 kifungu kidogo 'a' cha mwenendo wa makosa ya jinai sura namba 20 na kusema kuwa maombi hayo yameambatana na kiapo cha mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Mwanza RCO.

"Tunaomba hayo kutokana na mjibu maombi kushtakiwa katika shauri namba 11/2022 la kusafirisha binadamu kinyume cha sheria chini ya kifungu namba 4 kifungu kidogo namba 1 (a) na kifungu namba 6 kifungu kidogo namba 11 (a) cha Sheria ya Udhibiti wa Usafirishaji Haramu ya mwaka 2016 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021/22.

Kutokana na sheria hiyo, alimtaka Zumaridi kuweka saini na kukubali maombi hayo mbele ya mahakama na kuahidi kuwa mwenye tabia nzuri, atatunza amani na  hatosababisha fujo yoyote kwa kipindi hicho cha miaka mitatu.

Saa 8:23, Hakimu Lema aliahirisha kikao hicho kwa muda wa dakika 30 kumpa nafasi Zumaridi kujifikiria na kutoa uamuzi kama atakubaliana nayo bila kuwapo kwa wakili utetezi kutokana na shauri hilo kuitwa kwa dharura.

Baada ya kurejea katika kikao hicho, upande wa utetezi ulifika na wakili wa utetezi, Erick Muta, na kukubaliana na baadhi ya maombi kwa njia ya mdomo huku akieleza kuwa baadhi ya maombi yaliyotolewa yanaondoa haki ya msingi ya kikatiba ya kuwa huru kutokana na maombi hayo kujengwa katika msingi wa shaka na hofu na kumnyima mpokea maombi kuwa huru wakati wa maisha yake uraiani.

Wakili Akyoo alidai lengo la kufikisha ombi hilo ni kwa ajili ya kumfanya mjibu maombi (Zumaridi) asijihusishe na vitendo ambavyo awali alishtakiwa nayo.   Baada ya maelezo hayo,  Hakimu Lema aliahirisha utolewaji wa majibu ya maombi hayo huku akiwataka kurejea mahakamani Februari 14 kwa ajili ya kusikiliza majibu ya maombi hayo.

Pamoja na kuachiwa huru, Zumaridi anaendelea kutumikia kifungo cha mwezi mmoja na zimesalia siku 10 kumaliza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live