Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Zuieni mbwa wenu kuzurura ni hatari’

A548d7cd751affb21f82a797ebfeb108.jpeg ‘Zuieni mbwa wenu kuzurura ni hatari’

Fri, 2 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

OFISA Afya wa Mkoa wa Manyara, Mabula Masunga, amewataka wanaofuga mbwa wasiruhusu wanyama hao kuzurura porini ili kuwaepushia hatari ya kung’atwa na wanyamapori na kupata ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Alisema ili kuepuka ugonjwa huo wa mlipuko, wafugaji wa mbwa watumie utaratibu mzuri wa kuwafungia mbwa nyumbani ili wasiende kuzunguka porini ambapo ni rahisi kupata ugonjwa huo.

Alisema ugonjwa huo unaenezwa na wanyama wa porini na mara nyingi unadaiwa kuenezwa na popo wa porini ambao huwang’ata wanyamaporini kisha wanyama hao kuwang’ata mbwa na mbwa nao kueneza kwa kuwang’ata binadamu.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, moja ya ishara za mbwa kupata kichaa cha mbwa ni pamoja mbwa kuduwaa kwa muda mrefu sehemu moja kama anayewinda mtu.

“Hali hiyo hutokea siku saba baada ya mbwa kung’atwa na mnyamapori mwenye ugonjwa huo,” alisema na kutaja dalili nyingine kuwa ni pamoja na kuogopa maji kwani anapoyaona hubweka kwa kuogopa.

“Kwa binadamu akishaambukizwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa, naye huanza kubweka kama mbwa,” alisema Mabula na kuongeza: “Dalili zinapoanza kujitokeza, binadamu na yeye huogopa kunywa maji au kuona maji sehemu yeyote ile lakini pia anakuwa anauma binadamu wenzake hali inayowafanya hao walioumwa nao kuambukizwa.na kushamuuma binadamu mwenzake naye hupatwa na ugonjwa huo,” alisema.

Masunga alisema ili kuzuia na ugonjwa huo, wanyama wanapaswa kupewa chanjo na kuwaua wanaozurura ovyo hasa wenye dalili za kichaa cha mbwa ili kuzuia wasiwaume na kuambukiza binadamu.

“Serikali inafanya jitihada ya kuwaua, lakini baada ya muda wanaongezeka kwa kasi na hii ni kwa sababu ukimpiga mmoja, wengine wanakuwa wameshajua wanaenda kujificha na baada ya muda, wanatoka,” alisema.

Mkazi wa Babati, Pascalina Massey, alisema ongezeko la mbwa mtaani ni hatari hususani kwa watoto wadogo kwani ni rahisi kung’atwa na mbwa wanaozurura ovyo na kupata ugonjwa huo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz