Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zimamoto watoa darasa kwa wakulima korosho

C17ec28fac42928f26e9424431b13b3d Zimamoto watoa darasa kwa wakulima korosho

Mon, 14 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHI la Zimamoto na Uokoaji mkoani Mtwara limetoa elimu kwa wataalamu wa zao la korosho mintarafu namna ya kupambana na moto katika mashamba yao.

Zimamoto walitoa elimu hiyo hivi karibuni katika kikao cha siku mbili cha tathimini ya utekelezaji wa kazi za utafiti zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) kwa mwaka 2019/2020.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Mtwara, Christina Sunga, alisema moto wa porini huathiri zaidi mimea shambani.

Aliwataka wenye mashamba makubwa zaidi ya ekari 10 kulima njia za moto ndani ya mashamba yao kwa kutengeneza kipande kimoja kwa kipande kingine na njia za ndani ya shamba ziwe na urefu au upana usiopungua mita tano hadi sita.

Alisema njia zinazotenganisha shamba na shamba zinapaswa kuwa na upana wa mita 10 kwa kuwa barabara zinaweza kutumika baadaye kwa uvunaji na usafirishaji wa mazao kwa kutumia magari au guta.

“Moto unapotokea, unaweza kukadiria kipande ambacho hakijaathirika kwa kulima mtaro utakaozuia moto kuenea kutoka eneo moja kwenda lingine na hivyo, kusalimisha eneo la shamba lililosalia,” alisema.

Akaongeza: “Wakati wa palizi, badala ya kuchoma takataka, ni vyema zikatengenezwa mbolea aina ya mboji na hivyo, kuepusha shamba kuteketea kwa moto na kuharibu rutuba.”

Kamanda Sunga aliwataka wakulima na jamii kwa kwa kuhakikisha wanazima moto unaotumika kwa shughuli mbalimbali zikiwamo za upishi baada ya matumizi.

Chanzo: habarileo.co.tz