Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zaidi ya mifuko 600 ya saruji iliyoibwa yadakwa

Saruji Picsz Zaidi ya mifuko 600 ya saruji iliyoibwa yadakwa

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: Mwananchi

Zaidi ya mifuko 600 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya Sh20 milioni inayodaiwa kuibiwa katika mradi wa ujenzi wa shule ya wasichana ya Mkoa wa Mara, imepatikana ikiwa imehifadhiwa katika nyumba moja katika kijiji cha Karukekere umbali wa zaidi ya kilomita 15 kutoka eneo la mradi.

Shule hiyo inayojengwa katika kijiji cha Bulamba wilayani Bunda, inatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh4 bilioni huku Serikali ikiwa imeshatoa Sh3 bilioni.

Akizungumza jana kijijini Karukekere baada ya kuiona mifuko hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano alisema tukio hilo ni la aibu na halikubaliki.

“Hii saruji iliyohifadhiwa humu tumejiridhisha pasipo na shaka ni mali ya Serikali kwa sababu kwanza miradi ya Serikali inajengwa kwa saruji yenye kiwango cha 42.5, tofauti na ile saruji ya mtaani ambayo ni 32.5.

“Pia saruji ya Simba imeadimika mtaani na sisi tulitoa oda moja kwa moja kiwandani, lakini pia mazingira tuliyoyakuta hapa ni kiashiria tosha huu mzigo ni wa wizi,” alisema.

Alifafanua mzigo huo wa saruji ambao bado haujajulikana namna uliondolewa eneo la mradi, ulifikishwa kijijini hapo Oktoba 24, saa 9 alasiri na ulikuwa umeanza kuuzwa kwa Sh21,000 kwa mfuko tofauti na bei ya jumla ya Sh24,000.

Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa wilaya aliagiza kukamatwa kwa mmiliki wa nyumba iliyotumika kuhifadhi mifuko hiyo, huku msako ukiendelea wa kumtafuta mdogo wa mmiliki huyo, Maise Magesa anayedaiwa kuleta mzigo huo katika eneo hilo.

“Naamini kuna watu wetu wanahusika moja kwa moja kwenye hili tukio, sasa tumeanza uchunguzi sambamba na ukaguzi wa vifaa vyote kila kitu tutaangalia tulinganishe kile kilichoketwa na kile kilichotumika hatutasamehe hata msumari mmoja, lazima hii tabia ikomeshwe," alisisitiza

Awali, akizungumza kabla ya kukamatwa mtuhumiwa wa kwanza, Nyandago Magesa alisema hajui chochote kuhusiana na saruji hiyo kwa maelezo kuwa saruji hiyo ililetwa na mdogo wake.

Wakisimulia tukio hilo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Karukekere walisema walishuhudia mzigo wa saruji ukishuswa kwenye nyumba hiyo bila lujua kama ni mali ya wizi.

"Mzigo wa kwanza ulishushwa saa 9 mchana na baadaye mingine ilifuata, lori lilishusha mzigo mara nne na tulijua mwenzetu amefungua biashara mpya," amesema Joshua Deya.

Boniface Maiga, aliitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaohujumu miradi kwa maelezo kuwa tabia hiyo inasababisha miradi kutokuwa na thamani ya fedha halisi.

Chanzo: Mwananchi