Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zaidi ya Bil. 1.6 zakamilisha miradi ya elimu Ukerewe

Zaidi Ya Bil. 1.6 Zakamilisha Miradi Ya Elimu Ukerewe.png Zaidi ya Bil. 1.6 zakamilisha miradi ya elimu Ukerewe

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zaidi ya shilingi bilioni 1.6 zimekamilisha ujenzi wa miradi ya elimu katika shule za msingi kupitia mpango wa BOOST katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, hatua ambayo itawaondoa adha ya wanafunzi katika mwaka ujao wa masomo unaonza mwezi Januari 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Shelembi amesema miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vyumba 50 vya madarasa, matundu 68 ya vyoo, madawati 660, viti 140, majengo mawili ya utawala na nyumba moja yenye muundo wa kutumika na waalimu wawili (2 in 1).

Shelembi amezitaja shule zilizonufaika na miradi hiyo kuwa ni pamoja na Murutilima, Nakasahenge, Mandela, Nyerere, Kalendelo, Mulezi, Namagubo, Bugorola pamoja na shule mpya za Kivukoni na Kilimabuye.

“Katika sekta ya elimu tumepunguza adha kwa wanafunzi wetu, hasa kutembea umbali mrefu kutoka visiwani jambo ambalo ni hatari ziwani. Pia itaondoa msongamano changamoto ya msongamano wa wanafunzi darasani kutoka wanafunzi 120 hadi 45” amesema Shelembi.

Amebainisha kuwa kati ya shilingi bilioni 1,670,700 zilizopokelewa kupitia BOOST, miradi iliyokusudiwa imekamilika kwa ubora na kufakiwa kubakiza chenchi ya shilingi milioni 60 pamoja na vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 10 zitakazoelekezwa kuboresha miundombinu yenye changamoto.

Pia Shelembi ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali za wananchi na kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya.

“Kwa miaka miwili 2021/22 na 2022/23 tumepokea jumla ya shilingi bilioni 20.258 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Ni kazi kubwa inafanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo kazi yetu ni kumsaidia kwa kazi nzuri anayoifanya kwa watanzania” amesema Shelembi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukerewe, Joshua Manumbu katika kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Halmashauri hiyo imesimamia kwa asilimia 100 bajeti yake na kufanikiwa kukamilisha miradi ya wananchi ikiwemo zahanati, vituo vya afya na madarasa.

“Kipekee kabisa nimpongeze sana DC aliyepita (Denis Mwilla), Mungu ambariki huko Mbarali. Tulifanya kazi pamoja tukishirikiana na Mkurugenzi Shelembi na Kamati ya Siasa ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile. Tumetekeleza miradi yote kwa ubora na hakuna mradi uliokwama baada ya kupitiwa na mwenge” amesema Manumbu na kuongeza;

“Lakini pia nimpongeze Mhe. DC Hassan Bomboko ambaye bado ana muda mfupi Ukerewe, tunaona ufuatiliaji wake wa miradi ni mzuri, tuendelee kushirikiana ili kusimamia fedha za miradi ya maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25” amesema Manumbu.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile amesema Serikali iko kazini na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25 inatekelezwa.

“Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, Mkurugenzi Emmanuel Shelembi amekuwa ni mfano wa watendaji bora katika kusimamia miradi ya maendeleo” amesema Mambile. Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Hassan Bomboko amesema miradi ya maendeleo ikiwemo ya elimu imetekelezwa kwa ubora katika Wilaya hiyo na kukamilika kwa asilimia 100 ikiendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live