Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yaliyojitokeza mazishi ya Mengi

Video Archive
Mon, 13 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Ni dhahiri kwamba aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi hatutamuona tena na itabaki kuwa historia na kumbukumbu ya yale ambayo ameyafanya enzi za uhai wake, baada ya juzi Mei 9, 2019 kupumzishwa katika nyumba yake ya milele Machame mkoani Kilimanjaro.

Haya ni sehemu ya mambo yaliyojitokeza katika msiba wake mkoani Kilimanjaro wakati wa mapokezi ya mwili wake hadi kuzikwa.

Mapokezi uwanja wa Kia

Haijapata kutokea, hivi ndivyo unavyoweza kusema kutokana na umati mkubwa uliojitokeza katika mapokezi ya mwili wa Mengi.

Mwili huo uliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Mei 8, 2019  kisha msafara ukaanza kuelekea nyumbani kwake kijiji cha Nkweseko wilaya ya Hai, mkoani hapa.

Mwili huo ulipokewa na umati wakiwamo viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali mkoa wa Kilimanjaro, wakiongozwa na  mkuu wa mkoa huo, Anna Mghwira na viongozi walioambatana nao kutokea Dar es Salaam akiwamo Paul Makonda mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na Christopher ole Sendeka, mkuu wa mkoa Njombe.

Pia Soma

Baada ya mwili huo kuwasili kwa ndege ya shirika la Precisionair uliingizwa kwenye gari lililopambwa kwa mashada ya maua huku katika vibao vya namba mbele na nyuma vikiwa nimeandikwa R.I.P Reginald A. Mengi kisha msafara kuanza kueleka kijiji cha Nkweseko.

Watu walivyozuia msafara

Baada ya msafara huo kuanza ulikutana na maelfu ya wananchi waliokuwa wamejipanga barabarani kuulaki mwili huo, huku wengine wakilia kwa uchungu.

Mapokezi yalikuwa ni makubwa ya wananchi ambao wengine walikuwa wakisukumana kugusa gari lililokuwa limebeba mwili huo huku baadhi ya kina mama wakitandika khanga barabarani na wengine wake kwa waume, vijana na watoto wakiwa wamebeba matawi ya miti kuonyesha heshima na upendo kwa mfanyabiashara huyo maarufu aliyefariki dunia Mei 2 akiwa Dudai, Falme za Kiarabu.

Kuanzia eneo la Bomang’ombe watu waliongezeka barabarani hali iliyowapa polisi wakati mgumu na kumlazimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah kushuka kwenye gari na kusaidiana na askari wengine kuondoa watu barabarani ili msafara huo uendelee.

Msafara wazuiwa

Msafara huo uliokuwa na magari zaidi ya 20, baada ya kufika kijiji cha Nkwarungo Machame, wananchi waliuzuia na kutaka jeneza lishushwe ili waweze kulibeba hadi nyumbani katika kijiji cha Nkweseko.

Msafara huo ulilazimika kusimama kwa saa moja ili kuondoa wananchi waliokuwa barabarani wakipiga kelele kutaka mwili ushushwe wambebe na baada ya polisi kuwaondoa msafara uliendelea.

Nyumba ya Mengi ilivyozua gumzo

Msafara uliokuwa na mwili wa Mengi ulifika nyumbani kwake katika kijiji cha Nkweseko alasiri na kisha kuingizwa katika nyumba ya kifahari iliyopo katikati ya msitu.

Nyumba hiyo ilionekana kuwa kivutio kwa watu wengi waliofika eneo hilo na hata kwenye mitandao ya kijamii ambako picha za nyumba hiyo  zimesambaa na kuzua gumzo kutokana na muonekano wake na mazingira yanayoizunguka.

Barabara zilivyofungwa

Barabara zote za kuingia na kutoka katika kanisa kuu la Usharika wa Moshi mjini wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) zilifungwa kwa kuwekewa utepe wa njano na polisi wakati wa ibada ya mazishi ya Mengi kutokana na umati uliojitokeza.

Barabara ya kuelekea kanisa hilo ukitokea ofisi ya mkuu wa mkoa Kilimanjaro ilifungwa kuanzia jengo la NSSF Commercial Complex, wakati ile ya kutokea barabara ya Boma kuelekea kanisani ilifungwa kuanzia ilipo benki ya KCB.

Halikadhalika, barabara zinazoingia katika kanisa hilo kutokea eneo la kituo kikuu cha mabasi nazo zilifungwa huku polisi wa trafiki, wenye sare na wasio na sare wakiimarisha ulinzi kanisani hapo.

Hadi kufikia saa 3:30 asubuhi kanisa lilikuwa limefurika waombolezaji ndani na nje kwenye mahema, huku wengi wakifuatilia ibada hiyo nje ya uzio wa kanisa na eneo la meta za mraba 100 kuzunguka kanisa hilo.

"Sijawahi kuona umati mkubwa kiasi hiki katika kanisa letu. Hii inadhihirisha Mzee Mengi aliishi kwenye mioyo ya Watanzania," alisema Davis Mosha aliyewahi kugombea ubunge Jimbo la Moshi mwaka 2015.

Kauli ya Mbowe, Shoo na Bashiru zilivyotikisa

Akitoa salamu za rambirambi, mbunge wa (Chadema), Freeman Mbowe alisema inapotokea kiongozi fulani akatoa maneno ya kubeza kabila fulani, watu wanaanza kubaguana kwa kabila na dini kuna kwaza wengine.

“Kipekee kabisa, mnisamehe, niseme jambo moja ambalo limetukwaza wengi na kwa sababu sina tabia ya unafiki nitasema straight (moja kwa moja), kauli za kuambiana kuwa kuna kabila fulani haliwezi kuwatetea walemavu si za kweli, ni za kibaguzi ni lazima tuzikemee”alisema Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Kauli hiyo ya Mbowe iliungwa mkono na mkuu wa KKKT, Dk Fredrick Shoo akisema kama kuna dhambi ambayo binadamu wanapaswa kuifanyia toba ni ya kubaguana na kama Watanzania wanahitaji Taifa lipokee baraka kutoka kwa Mungu ni kuacha kufanya hivyo.

“Nimemsikiliza mbunge wetu Mbowe akisema jambo fulani ambalo wakati mwingine huenda tunaongea kwa ndimi kuteleza, tunaomba sana Mungu atusaidie, tusibaguane kwa misingi yoyote ile.”

Shoo alitumia pia nafasi hiyo kukemea viongozi vijana ambao alidai wamekuwa wakijitutumua, kauli ambayo ilionekana kuungwa mkono na wananchi waliokuwa kanisani kwa kupiga makofi na kushangilia.

Msiba huo wakutanisha viongozi mbalimbali

Msiba huo uliwakutanisha viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na wa dini mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki msiba huo ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa;  Spika, Job Ndugai, Waziri wa Uwekezaji Angella Kairuki; Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda; Waziri wa Ardhi, William Lukuvi na Waziri wa Mifugo, Luhaga Mpina.

Wingine ni wabunge kutoka maeneo mbalimbali akiwemo, wabunge wa kuteuliwa, Anna Kilango Malecela na Salma Kikwete; Nape Nnauye (Mtama), James Mbatia (Vunjo) pamoja na wakuu wa mikoa na wilaya.

Chanzo: mwananchi.co.tz