Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

YES TZ kutokomeza mimba za utotoni Rukwa

78feb26b6294b7f67f0866a227c9a118.png YES TZ kutokomeza mimba za utotoni Rukwa

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la YES Tz la jijini Mbeya limeungana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika mapambano ya kutokomeza ndoa na mimba za utotoni mkoani Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amerikaribisha shirika hilo, akisema takwimu za utafiti wa kidemografia za mwaka 2015/2016 zinaonesha asilimia 29 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 na 19 mkoani humo, wameshazaa au wajawazito.

Alisema takwimu za matukio ya mimba za utotoni katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2019, zinaonesha matukio 722 ya wanafunzi kupata mimba mkoani humo, ambayo kati yake 171 yalitokea katika shule za msingi na 551 katika shule za sekondari.

Alisema kwa kuzingatia Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, mwaka 2019 mkoa huo ulikadiriwa kuwa na wanawake 17,142 wenye miaka kati ya 15 na 19.

Hivyo, kwa kupitia takwimu za utafiti huo, maana yake kuna jumla ya wanawake 22,371 sawa na asilimia 29 wanaotekeleza jukumu la kulea watoto baada ya kujifungua au ni wajawazito.

Wakati kiwango hicho kikiwa kikubwa ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia 27, Wangabo alisema takwimu zinaonesha kuwa robo ya akinamama mkoani humo, wanaohudhuria hudhurio la kwanza katika kliniki kwa ajili ya huduma za wajawazito, wana umri chini ya miaka 20.

“Ukishirikiana na wadau mbalimbali, mkoa wa Rukwa umekuja na mkakati wa miaka mitano (Julai 2020 hadi Juni 2025) ulioanisha changamoto, kazi ya kufanyika, wahusika, mbinu za kutumika na muda wa utekelezaji katika kukabiliana na tatizo la mimba za utotoni”alisema.

Kwa kupitia ufadhili wa miaka mitano wa shirika la Plan International, Mkurugenzi wa YES Tz, Kenneth Simbaya alisema shirika lao litafanya kazi na wadau mbalimbali kufikisha elimu ya afya ya uzazi (SRH) kwa vijana ndani na nje ya shule.

Alisema mimba za utotoni ni miongoni mwa sababu zinazochangia vifo vitakanavyo na matatizo ya uzazi na vifo vya watoto wachanga na zina madhara mengine kiafya, kielimu, kiuchumi na kijamii.

Mratibu wa YES Tz katika mapambano hayo, Navina Mutabazi alitaja sababu zingine za ndoa na mimba za utotoni kuwa ni kutokuwepo usawa wa kijinsia na thamani ya chini wanayopewa wasichana.

Chanzo: habarileo.co.tz