Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizi mifuniko ya chemba za majitaka wakithiri Moshi

Moshiii 0117280 Wizi mifuniko ya chemba za majitaka wakithiri Moshi

Fri, 26 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) imewataka viongozi wa kata, mitaa na wananchi kutoa ushirikiano katika kulinda miundombinu ya maji na kudhibiti wizi wa mifuniko ya chemba za majitaka ili kuzuia kufurika kwa uchafu na kuenea kwa magonjwa ya milipuko.

Wito huo umetolewa leo, Januari 25, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Muwsa, Edes Mushi alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema wizi wa mifuniko ya chemba za majitaka kwa sasa ni changamoto kubwa.

Mushi amesema katika kipindi cha hivi karibuni, imeibiwa mifuniko ya chemba zaidi ya 15 na kuisababishia mamlaka hasara ya zaidi ya Sh13.5 milioni pamoja na kuhatarisha afya za wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Pia, amesema ni vema wananchi na viongozi wa mitaa wakatoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo, kuwabaini wanaohujumu miundombinu, ili kudhibiti changamoto hiyo na kuhakikisha mji unakuwa safi na huduma inakuwa bora na endelevu.

“Miundombinu ya maji taka kwa siku za karibuni hali si nzuri kwa sababu tuna mradi tumeujenga kutoka Korongoni kwenda kwenye mabwawa ya mabogini, mifuniko ya chemba za maji taka iliibiwa zaidi ya 15 na mifuniko ile gharama zake ni kubwa.

“Hiyo ni changamoto kubwa ambayo inasababisha takataka kuingia kwenye miundombinu ile na mwisho wa siku miundombinu inaziba na majitaka yanafurika juu, jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi,” amesema Mushi.

Mushi pia amewaomba wananchi kutoa taarifa za mivujo na wizi wa maji, ili kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 23 ya sasa hadi kufikia chini ya asilimia 20.

“Kwa sasa tunapoteza maji kwa asilimia 23, bado tunaendelea kudhibiti upotevu huu, kwani kiwango cha chini kinachohitajika ni asilimia 20 na tunahitaji tufike chini ya hapo. Tuombe wananchi waendelee kutupa taarifa kunapoonekana changamoto za mivujo na taarifa za wale wanaoiba kwa kuchezea mita au kutoboa bomba nyuma ya mita,” amesema.

Amesema katika kudhibiti changamoto hizo, kwa sasa wametangaza kutoa zawadi ya fedha kuanzia Sh100,000 kwa wananchi watakaotoa taarifa sahihi kuhusiana na uharibifu wa miundombinu na hata wizi maji.

Mkazi wa Moshi, Perepetua Kimaro amesema wizi wa mifuniko ya chemba ni tatizo linalohitaji kudhibitiwa kwa nguvu zote, ili kuepusha magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu.

“Muwsa imekuwa ikifanya kazi kubwa kudhibiti maji taka, lakini kumekuwepo na baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaiba mifuniko, na hili ni tatizo katika maeneo mbalimbali, tuombe Muwsa waendelee kulidhibiti ili kuimarisha usafi wa mji wa Moshi,” amesisitiza Kimaro.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live